Wadau waliohudhuria Uzinduzi wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto(PJT-MMMAM) ngazi ya Halimashauri ya Wilaya ya Mbeya wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya uzinduzi huo(Picha na Joachim Nyambo).
Na Joachim Nyambo, Mbeya.
WAZAZI wilayani hapa wamehimizwa kuwapeleka watoto katika vituo vya kutolea huduma za Afya watoto wanaozaliwa pale wanapobaini wana changamoto mbalimbali ikiwemo ulemavu ambao haukufahamika mapema baada ya mtoto kuzaliwa.
Kadhalika wazazi hususani wanawake waliojifungua wameatakiwa kuzingatia ratiba za mahudhurio ya kliniki wanazopangiwa baada ya kujifungua na kuruhusiwa kurudi majumbani kwao ili kuwapa nafasi wataalamu kujua maendeleo ya awali ya watoto wao.
Mratibu Msaidizi wa Afya ya Mama na Mtoto katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Martha Macha alibainisha hayo kwenye uzinduzi wa ngazi ya Halimashauri wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto(PJT-MMMAM).
Macha alisema pamoja na wataalamu wa Afya kutumia muda wa kutosha kuwakagua watoto wachanga mara baada ya kuzaliwa zipo changamoto ikiwemo baadhi ya aina za ulemavu zinazoweza kubainika wakati mama aliyejifungua amekwisharuhusiwa kurudi nyumbani.
Alisema ni muhimu kwa mzazi husika au jamii inayomzunguka kuchukua hatua za haraka kumrudisha mtoto huyo katika kituo alichopata huduma ya kujifungua ili wataalamu waweze kumchunguza zaidi na kumpa huduma stahiki.
Alisema kuchelewa kutoa taarifa kwa watoa huduma za Afya na pia kutozingatia ratiba za mahudhurio ya kliniki wanazopewa wanawake baada ya kujifungua kunaweza kumsababishia mtoto husika changamoto aliyonayo kuwa kubwa zaidi na kama ni ulemavu kuwa wa kudumu ili hali angeweza kusaidiwa mapema angeondokana nao.
“Watalamu tunajitahidi kwa kiasi kikubwa kufanya ukaguzi wa mtoto anapozaliwa. Yawezekana zikawepo changamoto ambazo tunaweza tusizigundue kwa haraka japo ni mara chache sana kutokea.
Tunachoshauri ni iwapo wazazi wanabaini changamoto yoyote basi warudi haraka kwenye kituo walichopata huduma ya kujifungua.” Alisema Macha.
“Lakini pia mara baada ya mama kujifungua kuna tarehe anazopangiwa arudi kliniki zile nazo ni muhimu kuzizingatia kwakuwa ni siku zinatumiwa pia na wataalamu kuweza kuangalia mwenendo wa mtoto aliyezaliwa. Kama kuna changamoto ambayo haikubainika awali wanaweza kuiona na kuifanyia kazi.” Aliongeza.
Kadhalika mratibu huyo msaidizi wa Afya ya Mama na Mtoto alisisitiza wajawazito kuhudhuria kliniki na pia kujifungulia kwenye vituo vya utoaji huduma za Afya na iwapo inatokea kwa bahati mbaya wanajifungulia majumbani wawahishwe kwenye vituo hivyo ili huduma muhimu ikiwemo ukaguzi wa kitabibu ufanyike kwao na watoto wanaozaliwa.
Mmoja wa wazee maarufu kutoka Kata ya Iwindi wilayani hapa, Harison Nswila alisema elimu juu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto(MMMAM) bado inahitajika kwa kiasi kikubwa kwa jamii kwakuwa zipo changamoto zinawakabili watoto walio na umri wa kati ya miaka sifuri hadi nane kutokana na wazazi au jamii kukosa uelewa.
Mzee Nswila alisema upo ulemavu kwa watoto unaotokana na kukosekana kwa umakini wakati watoto wanapozaliwa hivyo ni muhimu wazazi wakawa na elimu ya sifa anazopaswa kuwa nazo mtoto anapozaliwa.
“Mfano mzuri tunaambiwa mtoto anapozaliwa lazima alie akitoa sauti sasa kama hakulia lazima wewe mwenyewe ujue hiyo inaashiria nini.. ni kwamba huyo mtoto ana matatizo. Lakini elimu pia lazima itolewe wale wanaojifungulia kwa wakunga wajue kwamba pindi tu wanapojifungua wafike katika Zahanati zilizopo kwenye vijiji vyao kwaajili ya kupata utaalamu zaidi juu ya malezi ya watoto. Alisema Mzee Nswila.”
Mratibu wa Mradi wa Mtoto Kwanza unaoichechemua PJT-MMMAM kutoka Shirika lisilo la kiserikali la Shalom, Jenipher Antony alisema kikao hicho cha uzinduzi kilionesha muitikio chanya kwa wadau waliohudhuria kuahidi kuhakikisha jamii inapata elimu ya kutosha.
Antony alisema PJT-MMMAM inahitaji ujumuishi kwenye utekelezaji wake hivyo kila mdau analo jukumu la kuhakikisha wazazi na jamii kwa ujumla wanatambua mambo ya msingi yanayowezesha mtoto kuwa na ukuaji timilifu.
Awali akifungua kikao hicho, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halimashauri ya Wilaya ya Mbeya, Agnes Elikunda alisisitiza kila mdau kutumia eneo lake kuhakikisha jamii inashiriki kwenye utekelezaji wa Programu ambayo serikali iliianzisha baada ya kuona kuna uwekezaji mdogo kwenye eneo la makuzi ya watoto walio katika umri wa miaka sifuri hadi nane.