Serikali imeeleza leo
kwamba, Uhusiano kati ya Misri na Zanzibar umeendelea kukua na kuimarika licha
ya Serikali ya Misri kufunga Ubalozi wake mdogo Zanzibar kwenye miaka ya 1990.
Hayo yalielezwa Bungeni
leo na Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki alipokuwa akijibu Swali la nyongeza la Mhe. Ali
Juma Mohamed, Mbunge wa Shaurimoyo, aliyetaka kujua sababu za nchi ya Misri
kufunga Ubalozi wake Mdogo Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Waziri
alifahamisha kwamba Misri haikutoa sababu za kufunga Ubalozi wake mdogo
Zanzibar. Hata hivyo, alieleza zaidi kuwa pamoja na kufungwa kwa ofisi hizo,
mahusiano na ushirikiano kati ya Misri na Zanzibar yameendelea kukua na
kuimarika siku hadi siku kupitia Ubalozi wake uliopo Dar es Salaam.
Awali, katika suala
lake la msingi, Mhe. Mohamed alitaka kujua idadi ya Balozi ndogo zilizopo
Zanzibar, ambapo alijibiwa kuwa hadi kufikia Agosti, 2023, nchi zilizofungua
Ofisi ndogo za Ubalozi Zanzibar ni China; India; Msumbiji; Oman na Umoja wa
Falme za Kiarabu (UAE).
Aidha, Mheshimiwa Naibu
Waziri alieleza kuwa suala la kufungua na kufunga Ubalozi ni suala la kawaida katika
ulimwengu wa Kidiplomasia. Alitaja sababu za nchi kufunga
Ubalozi kuwa ni pamoja na; Kutetereka au kuharibika kwa mahusiano ya nchi
husika; nchi kubadili mwelekeo wa kimaslahi na kistrategia; kukosekana kwa
usalama katika nchi husika; na mwisho ni hali ya kiuchumi ambapo nchi hufunga
Ubalozi au Konseli Kuu kwa ajili ya kubana matumizi.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akijibu swali Bungeni jijini Dodoma |
Waheshimiwa Wabunge wakisikiliza majibu ya swali kutoka kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk |