………..
Rais wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujeruman Mhe. Dkt Frank Walter Steinmeier anatarajiwa kutembelea Makumbusho ya Kumbukumbu ya Vita vya MajiMaji Songea tarehe 1 Novemba 2023.
Makumbusho hayo yana historia kubwa ya Vita vya MajiMaji wakati wa harakati za ukombozi dhidi ya ukoloni wa Wajerumani.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe. Kanali Laban Thomas amesema maandalizi ya kuupokea ugeni huo yamekamilika ambapo baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Songea ataenda moja kwa moja katika Makumbusho hiyo ya Vita vya MajiMaji.
Amesema akiwa katika Makumbusho hiyo atapata historia ya makumbusho hiyo na kutoa heshima kwa mashujaa waliokufa katika vita hivyo vilivyopiganwa mwaka 1905- 1907.
Kanali Thomas ameongeza kuwa pamoja na kutoa heshima kwa mashujaa wa Vita vya Majimaji, Rais huyo wa Ujerumani atakutana na baadhi ya wahanga wa vita hivyo na kutembelea Shule ya Msingi MajiMaji.
Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Kamshna Benard Wakulyamba amesema Wizara ya Maliasili na Makumbusho ya Taifa wanaosimamia Makumbusho ya MajiMaji wamekamilisha maandalizi kwa ajili ya kumpokea Rais huyo wa Ujerumani.
Mhe. Dkt. Frank-Walter Steinmeier yupo nchini kwa Ziara ya Kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 30 Oktoba hadi tarehe 01 Novemba 2023.
Ziara hii mbali na kudumisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa kimaendeleo kati ya Tanzania na Ujerumani, pia imelenga kukuza na kuimarisha misingi ya biashara nauwekezaji.