RAIS wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier akizungumza na waandishi wa habari Ikulu Far es salaam Leo Jumanne Oktoba 31, 2023 kuhusu ushirikiano wa masuala mbalimbali ambapo aliongozana na Mwenye wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. SAMIA Suluhu Hassan.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. SAMIA Suluhu HassanHassan akizungumza na waandishi wa habari Ikulu Far es salaam Leo Jumanne Oktoba 31, 2023 kuhusu ushirikiano wa masuala mbalimbali ambapo aliongozana na mgeni wake RAIS wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza kwenye Mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu ziara ya mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani Mhe. Dkt. Frank-Walter Steinmeier nchini Tanzania. Mkutano huo na Waandishi wa Habari umefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 31 Oktoba, 2023.
Wageni mbalimbali waliohudhuria Mkutano wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani Mhe. Dkt. Frank-Walter Steinmeier pamoja na Waandishi wa Habari Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 31 Oktoba, 2023.
PICHA JOHN BUKUKU NA IKULU -DAR ES SALAAM
……………………….
RAIS wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendesha nchi katika misingi ya kidemokrasia, utawala bora, sheria na haki za binadamu.
Aidha, Rais Steinmeier ameshauri Tanzania ilekeze nguvu kwenye nishati jadidifu na uchumi wa kidigitali ili kuweza kuchochea uchumi, huku akiweka bayana kuwa Ujerumani itashiriki kufanikisha hayo.
Rais Steinmeier amesema hayo leo Ikulu jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo ameweka bayana kuwa amefanya ziara hiyo ya kikazi ili kudumisha ushirikiano kati ya nchi hizo ambao una zaidi ya miaka 60 sasa.
Alisema wananchi wa Ujerumani wanaridhishwa na uongozi wa Rais Samia ambao unazingatia demokrasia, utawala bora, sheria na haki za binadamu, hivyo wataendelea kumuunga mkono hasa katika miradi ya maendeleo.
“Hii ni mara ya tatu nakuja Tanzania kusema kweli uongozi wa Rais Samia unawagusa wananchi wa Ujerumani, hivyo sisi tutahakiksha yale ambayo tunakubaliana yanatekelezwa na pande zote mbili ziweze kufaidika,” alisema.
Kwa upande mwingine Rais Steinmeier ameishauri Tanzania kuwekeza katika nishati jadidifu hali ambayo itawezesha kuwepo kwa nishati ya umeme ya uhakika, safi na salama kwa binadamu na mazingira.
Amesema Ujerumani itashiriki kutoa elimu kuhusu umuhimu wa nishati hiyo ambayo ndio kimbilio la dunia kwa sasa kutokama na mchango wake kwenye utunzaji wa mazingira.
Rais huyo amesema nishati jadidifu ni safi na salama, ila kubwa zaidi inachangia kukuza uchumi wa nchi kwa haraka kutokana na ukweli kuwa ikipatikana uendeshaji wake hauna gharama.
Aidha, Rais Steinmeier ametaja eneo lingine ambalo Tanzania kuweka mkazo ni kwenye uchumi wa kidigitali ambao unahusisha kundi kubwa la vijana.
“Sisi kwetu tumewekeza kwenye uchumi wa kidigitali, tumeambiwa hapa kuna vijana wabunifu wa Startup, nitakutana nao, ili tuzungumze namna ya kuwawezesha zaidi ili wawe wawekezaji wakubwa,” amesema.
Amesema uchumi wa kidigitali unawezesha vijana kupata ajira, hivyo ni vema eneo hilo likaungwa mkono kwa nguvu zote, kwa kuwa unaenda kuleta mapinduzi ya kiuchumi.
Rais huyo amesema Ujerumani itaendeleza ushirikiano na Tanzania katika sekta mbalimbali, lengo likiwa ni kuchochea maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Steinmeier amesema katika kudumisha ushirikiano leo atafanya ziara mkoani Ruvuma ambapo atakutana na ndugu na wapiganaji wa vita ya Majimaji na kuzungumza nao, huku akiahidi kufanya mchakato wa mabaki ya wapiganaji hao yaliyopo nchini Ujerumani yarejeshwe nchini Tanzania
“Katika ziara yangu hii kesho (leo) nitaenda Ruvuma, nitakutana na wapiganaji wa Vita ya Majimaji naamini tutaeleewana na kuona namna ya kurejesha mabaki ya ndugu zao yaliyopo nchini kwetu,” alisema.
Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha Rais Steinmeier, Rais Samia amesema Ujerumani na Tanzania zina historia ndefu katika sekta ya kilimo, afya, elimu, maji, biashara, mazingira, udhibiti fedha na nyingine, hivyo ziara hiyo inaenda kuongeza kasi zaidi ya mashirikiano hayo.
Rais Samia alisema Ujerumani imetekeleza miradi 180 ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika uchumi na huduma za kijamii zinazogusa watu wengi.
Amesema mwaka 2024 Tanzania itaandaa kongamano la majadiliano na Ujerumani ambapo matarajio yao ni kuhakikisha uwekezaji wa nchi hiyo unaongezeka zaidi.
Samia ameipongeza Taasisi ya Frankfurt Zoological Society kwa kuhifadhi mazingira katika maeneo mbalimbali na kuiomba Ujerumani kuendeleza mpango huo.
Pia amesema Ujerumani imewezesha wanawake wengi kiuchumi katika kipindi cha miaka 60 ya ushirikiano wao, hivyo matumaini yake ni kuona nguvu inaongezeka zaidi.