TAASISI na Vyuo Vikuu wamewasilisha mawasilisho 22 ya Maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa HEET, katika kikao kazi cha mradi wa mageuzi ya Kiuchumi kwa Elimu ya Juu.
Mawasilisho hayo yamewasilishwa katika kikao kazi cha Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (WyEST) ikishirikiana na Benki ya Dunia kilichohitimishwa jijini Dar es Salaam, tarehe 30 Oktoba, 2023 katika ukumbi wa Ndaki ya TEHAMA.
Katika kikao hicho Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (WyEST) kupitia Kitengo cha Usimamizi Mradi Kitaifa (NPIU) iliwasilisha maendeleo ya utekelezaji kwa nyanja ya majenzi, mapitio na uandaaji wa mitaala katika digrii programu kwenye maeneo ya vipaumbele (priority disciplines).
Pamoja na hayo masuala ya ulinzi wa mazingira na Jamii (environmental and social safeguards), taarifa ya fedha, na viashiria vya matokeo (result framework indicators) yalijadiliwa.
Akihitimisha kikao kazi hicho, Mratibu wa Mradi Ngazi ya Kitaifa ambaye pia ni Mkurugenzi wa Elimu ya Juu, Dkt. Kenny Hosea amezitaka Taasisi na Vyuo Vikuu kuongeza kasi ya kutekeleza mradi kwa kuzingatia taratibu za nchi na za Benki ya Dunia, na ubora wa majengo ili pawe na thamani ya fedha (value for money).
Kwa upande wa uwakilishi wa Benki ya Dunia ulitumia kikaokazi hicho kukumbushia mambo mbalimbali ya kuzingatia wakati wa kutekeleza majenzi. Baadhi ya mambo hayo ni pamoja na kufuata utaratibu kabla ya kuanza majenzi.