Na Sophia Kingimali
Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) kimeitaka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuweka wazi mchakato wa uwekezaji wa Bandari kama ambavyo amefanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Hayo yamebainishwa Oktoba 30,2023 jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa ADC, Hamad Rashid Mohamed wakati wa akifungua Mkutano wa Bodi ya Uongozi Taifa wa chama hicho ambao umejadili agenda tisa ikiwamo namna ya kujipanga kwa ajili ya uchaguzi ujao.
Aidha Hamad amesema kuwa wakati wa mchakato wa uingiaji wa mkataba wa uwekezaji wa Bandari ya Dar es Salaam na DP World, Dkt. Samia ameweka wazi suala hilo na kusababisha kada mbalimbali kutoa maoni yao na yaliyokubalika yakaingizwa jambo ambalo ni la kupongezwa na inatakiwa pia kufanywa na Rais wa Zanzibar, Dkt Hussein Ally Mwinyi.
“Kwa namna ambavyo Rais Samia, ameweka wazi mkataba wa Bandari ya Dar es Salaam na DP World, ADC tunamuomba Rais wa Zanzibar naye aweke wazi suala la uwekezaji wa Bandari ya Zanzibar ili kuondoa minong’ono isiyohitajika kwa sasa katika kutafuta maendeleo ya nchi”amesema Hamad.
Pia amewapongeza wajumbe waliojitokeza kuwania nafasi mbalimbali katika chaguzi za maraudio ambazo zimefanikisha kukitangaza chama licha ya uchanga wake katika ulingo wa siasa na kufanikiwa kushika nafasi ya pili katika chaguzi hizo.
“Chaguzi hizi hazilkuwa rahisi na hususan kwa chama chetu ambacho wengi walifikiri kwamba hatuna nafasi, wakati tunajipanga kuingia katika chaguzi, baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa na Serikali waliniuliza, Hamad we unaingia uchaguzi mbona huna tawi huko.amesema na kuongeza
“Nikawaambia mtaona miujiza ya ADC ilivyo kwani haifanyi kazi kwa mikutano ya adhara, hakifanyi kazi kwa propaganda, kinafanya kazi kidigitali na mtaona maana ya kidigitali nini maana yake na kweli tukapata nafasi ya pili wakati hakuna mikutano ya adhara wala propaganda,” amesema.
Amesema kuwa katika chaguzi hizo hawakutukana mtu na matokeo yalionekana kwa kushika nafasi ya pili na kufafanua kuwa wananchi siku zote wanataka kuona ithibati ya uongozi ya chama na sera zinazoweza kutekelezeka.
Wakati huo huo amewataka wanaotaka kujiunga na ADC kwa ajili ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kuwa wanakaribishwa kwani wao wanachohitaji ni kupata watu wenye uwezo wa kufanya kazi, taaluma zao nasi fedha zao.
Akizunguza vita vilivyopo ukanda wa gaza kati ya Palestina na Israel, Hamad amesema kuwa ni wakati muafaka sasa Umoja wa Mataifa (UN), kuingilia kati mgogoro huo huku akiwaomba pande mbili zinagombana kuheshimu mikataba ya amani ya kimataifa ili kuifanya dunia iendelee kuwa na amani na utulivu.