Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng’I Issa (watatu kulia) akifurahia jambo na washiriki wa mkutano wa Mwaka wa jumuiya ya wafanyabiashara mwanawake wa kiislamu (Muslimah Boss Network), uliofanyika jijini Dar es Salaam jana. (Watatu kushoto) ni Mkurugenzi Mtendaji wa jumuiya ya ‘Muslimah Boss Network’, Bi. Zulfa Adam.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng’I Issa (wapili kulia) akizungumza na washiriki wa mkutano wa Mwaka wa Jumuiya ya wafanyabiashara mwanawake wa kiislamu (Muslimah Boss Network), uliofanyika jijini Dar es Salaam jana. (katikati) ni Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya ‘Muslimah Boss Network’, Bi. Zulfa Adam.
Na Mwandishi Wetu
KATUBU Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng’i Issa amewataka wanawake na vijana nchini kutumia TEHAMA kutangaza biashara zao ili kuyafikia soko kiurahisi na kutanua wigo wa biashara sambamba na kuongeza kipato..
Akizungumza kwenye Mkutano wa Mwaka wa Jumuiya ya wafanyabiashara wanawake wa Kiislamu (Muslimah Boss Network) Jijini Dar es Salaam jana, Issa alisema wanawake na vijana watumie zaidi teknolojia ya mitandao ya kijamii kuzitangaza biashara zao na kuteka masoko ya ndani na nje ya nchi.
“Kupitia mtandao wenu mnaweza kujengeana uwezo wa namna bora ya kukuza mitaji yenu nakufanya vizuri katika biashara na kamwe msikate tamaa. Tumieni teknolojia ya mitandao ya kijamii kujitangaza zaidi ili kuongeza tija kwenye biashara mnazozifanyfanya,” alisema Beng’i
Beng’i alisema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ilishaweka wazi dhamira yake ya kuwajengea uwezo na kuwainua kiuchumi wanawake na vijana ikiwemo kutoa mikopo kupitia halmashauri na hivyo wachangamkie fursa zinazojitokeza kwa kujikwamua kiuchumi.
“Nitoe rai kwa wanawake wafanyabiashara na wajasiriamali ambao bado hawajaanza kutumia teknolojia ya mitandao ya kijamii waanze kuzitumia teknolojia hizi kufungua zaidi biashara zao na kuwafiki masoko na watu wengi kwa mara moja,” alisema.
Kuhusu mitaji, Beng’i alisema kwa sasa kuna wigo mpana ambao umefunguliwa kupitia mashirika yasiyo ya kiserikali kwa njia ya uwekezaji ambapo mtu anapewa mtaji pasipo kuchukua mkopo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya ‘Muslimah Boss Network’, Zulfa Adam alisema mkutano huo wa mwaka umewakutanisha wafanyabiashara wanawake zaidi ya 200 kutoka ndani na nje ya nchi ikilenga kubadilishana uzoefu na kujengeana uwezo wa namna bora wa ufanyaji biashara na kuondokana na ufanyaji biashara wa mazoea.
“Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2020 kumekuwa na mafanikio makubwa, kwani hapo awali tulianza na wanachama 10 lakini tunaona mpaka kufikia sasa tunawanachama hai zaidi ya 100,” alisema na kuongeza kuwa bado uhamasishaji unaendelea ili kuvutia wanawake wengi kujiunga na mtandao huu,” alisema Adam.
Naye, Mshiriki wa mkutano huo, Rahma Jamal alisema kupitia jumuiya hiyo ameweza kutanua wigo wa wateja wake kutokana na elimu iliyotolewa na wakufunzi mbalimbali na hivyo biashara yake kuimarika.
“Kupitia jumuiya hii nimenufaika sana kwani nimepewa mafunzo mbalimbali ambayo yamesaidia kukuza na kutanua wigo wa ufanyaji biashara yangu. Na kupitia mkutano huu mwaka tumepewa mbinu bora za kutumia mitandao ya kijamii ili kuwafikia wateja wengi zaidi na kuwa na kipato endelevu, “ alisema Bi. Jamal.
Mkutano wa Mwaka wa jumuiya ya wafanyabiashara mwanawake wa kiislamu (Muslimah Boss Network), unalenga kujengeana uwezo na kukuza uelewa kuhusu biashara, za mtandaoni ikiwa na lengo la kuongeza ufikiaji wa soko na kukuza mbinu za kibiashara kupitia mitandao ya kijamii.