……………
Ujenzi wa Uwanja cha ndege wa Mtemere katika Hifadhi ya Taifa Nyerere wenye urefu wa Kilometa 1.8 unaotekelezwa na Mradi Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) unatarajiwa kuwa chachu katika kuongeza idadi ya Watalii pamoja na kuongeza pato la Taifa kupitia sekta ya Utalii nchini.
Hayo yamebainishwa na Mwakilishi wa Mradi wa REGROW katika Hifadhi ya Taifa Nyerere, Afisa Mhifadhi Daniel Mathayo ambapo amesema uwanja uliopo sasa una uwezo wa kupokea ndege 12 ambapo kukamilika kwa Ujenzi wa Uwanja mpya utakaokuwa na uwezo wa kupokea kwa wingi ndege kubwa ambazozitakuwa na uwezo wa kubeba abiria Zaidi ya 100 hatua itakayochochea ongezeko la mapato katika hifadhi hiyo.
“Ndege zinazoshuka katika kiwanja cha sasa zina uwezo wa kubeba abiria sio Zaidi ya 20, lakinimradi wa REGROE unatekeleza uwanja wa ndege ambacho kitakuwa kikubwa chenye uwezo wa kushusha ndege kubwa zenye uwezo wa kubeba abiria wengi zaidi ya 100, kwahiyo tunategemea kwamba utekelezaji uwanja wa Mtemere utakuwa chachu katika kuongeza idadi ya Watalii na pia kuongeza pato la taifa”-Amesema Bw. Mathayo.
Kwa upande wake Mhandisi Mshauri wa uwanja wa ndege wa Mtemere Edson Shayo kutoka Kampuni ya Howard amesema kuwa Mradi huo ulioanza Juni 12, 2023 unatarajiwa kukamilika Agosti 2024 na mpaka sasa mpaka umefikia asilimia 21.7.
Afisa Utawala na Rasilimali Watu kutoka kampuni ya CHICO inayotekeleza ujenzi wa Uwanja wa ndege kupitia mradi wa REGROW Bw. Oscar Owajwa amesema mradi huo umeweza kutengeneza ajira kwa watu 140 zikiwemo za moja kwa moja na za muda mfupi ambapo kwa kijiji cha Mloka takribani watu 20 wameweza kupata ajira.
Mmoja wa Rubani wa ndege zinazosafirisha Watalii Hifadhi ya Taifa Nyerere, Bw.Khalid Amarjit ameipongeza REGROW kwa kutekeleza ujenzi huo ambapo amesema kuwa kukamilika kwa uwanja mpya wa ndege kutawarahisishia wao kutopata changamoto kwa kuwa uwanja uliopo kwasasa ni mdogo.
“Uwanja mpya utakapokuwa umekamilika hatutapata shida ya kutua hapa, na kutakuwa hakuna changamoto yoyote na kampuni nyingi zitaongezeka kuleta watalii kuja kutalii katika hifadhii hii ya Nyerere. Tunamshukuru Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan na REGROW kwa ujenzi wa uwanja mpya mkubwa”-Bw.Khalid Amarjit.
Hifadhi ya Taifa Nyerere iliyopandishwa hadhi Novemba 29, 2019 ndiyo Hifadhi namba moja kwa ukubwa barani Afrika yenye kilometa za mraba 30,893 ambayo inakuwa kwa kasi kwa kupata ongezeko kubwa la idadi ya Wageni wanaoingia kutalii kutokea mataifa mbalimbali ambapo kwa mwaka 2022/2023 hifadhi hiyo ilipokea takribani Watalii 54,864 hatua iliyochangia kuingiza mapato ya Shilingi Bilioni 10.9.