Na Sophia Kingimali
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa anatarajia kuwa Mgeni rasmi kwenye mkutano mkubwa wa wadau wa Anga ambao watajadili mambo mbalimbali na
na namna walivyojipanga kuendeleza sekta ya anga na kuwa chachu ya uchumi wa Taifa ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 20 ya mamlaka ya Usafiri wa Anga TCAA
Hayo yamebainishwa leo Oktoba 29, 2023 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Nchini (TCAA), Hamza Johari wakati akizungumzia miaka 20 ya mamlaka hiyo ambapo amesema waliamua kuandaa mbio za TCAA Fun Run 2023 katika mbio hizo ambazo wakinbiaji watashiriki katika mbio za kilomita 5 na 10.
Amesema Mamlaka hiyo ilianzishwa mwaka 2003 kufikia mwaka huu imetimiza miaka 20 tangu kuanzishwa kwake hivyo wanaangalia miaka 20 walikotoka na 20 wanakokwenda.
“Kesho tunatarajia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kufungua mkutano wa wadau wa Anga na kusherekea miaka 20 ya TCAA na wadau wa anga kwa kutathimini mafanikio tuliyopata na changamoto zinazotukabili, “amesema Johari.
Amesema jukumu lao ni kuhakikisha wadau wa anga wanafanya shughuli kwa kufuata taratibu na sheria zilizowekwa.
Amesema watu walikuwa wanakimbia vizuri na walijiaanda na mbio hizo katika kuweka mwili vizuri na afya njema.
Ametoa wito kwa watanzania wote kujali sana afya zao kwa kula vizuri na kufanya mazoezi kwa sababu ni tiba na yawe sehemu ya maisha yetu.
“Tukiendelea kufanya mazoezi mara kwa mara tutaepukana na magonjwa nyemelezi ambayo yanaweza kuhatarisha afya zetu,” amesema .
Aidha amewashukuru wana TCAA na wadau wengine ambao wamewaunga mkono katika mbio hizo.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Ubungo, Hashim Komba amesema kuwa miaka 20 ya TCAA ni mageuzi ya Sekta ya anga.
“Leo tulikuwa tunasherekea miaka 20 ya TCAA kwa kukimbia mbio za TCAA Fun Run 2023 kufanya mazoezi ni kuimarisha afya ya akili zetu, “amesema Komba.
Amesema TCAA inatoa huduma kwenye viwanja vya ndege 15 nchi nzima na amempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha viwanja vya ndege.