Na Sophia Kingimali
MKURUGENZI wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi, amesema utiaji saini Mikataba Mahsusi ya Uwekezaji na Uendeshaji wa sehemu ya Bandari ya Dar es Salaam, baina ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya DP World ya Dubai kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma Octoba 22, 2023, haikuwa ni jambo la siri bali ni la wazi na lilihisisha watu wote.
Matinyi ameyasema hayo oktoba 29 jijini Dar es Salaam kwenye kikao na wahariri wa vyombo vya habari wakati akijibu swali.
Akijibu swali lililoulizwa na moja ya waandishi wa habari kuhusu uwazi wa mkataba huo amesema
“Hakukuwa na siri, Watu walipewa mialiko wakiwemo Waandishi ambao walipewa na usafiri kutoka katikati ya Jiji hadi Chamwino na kuwarudisha, walialikwa Viongozi wa Siasa wa CCM na Upinzani, Wazee wametoka Zanzibar wengine, Viongozi wa Dini na Watendaji mbalimbali wa Serikali, halikuwa tukio la siri na TV na Radio zilirusha LIVE matangazo.
“Walikuwepo Waandishi wa mitandao mbalimbali ya kijamii Mimi nilizungumza nao wengine wakanihoji, hotuba ya Mkurugenzi wa TPA ilieleza vitu kwa upana na urefu unaweza kurudi Youtube ukaisikiliza, hakukuwa na kitu cha kuficha, Rais alizungumza, Makamu wa Rais alizungumza na Watu wa DP World walizungumza , hakukuwa na usiri,”amesema.
Amefafanua kuwa “Sina uhakika kama hata kama umekwenda pale haukujua umealikwa kwa kitu gani kwamba utasema kulikuwa na usiri kwasababu umekiona ulichokiona, sidhani kama hiyo inatosha kusema jambo lilikuwa la siri kwasababu limewekwa wazi na kila Mtu ameliona,”amesema.
Amesema kampuni ya pamoja itakayoundwa kati ya Mamlaka ya Bandari (TPA) na kampuni ya DP World itasajiliwa nchini kwa lengo la kuendesha magati manne.
Amesema ipo haja ya watanzania kufahamu bandari ya Tanzania ni kitu gani na kuifahamu kwa kina ambapo endapo bandari hiyo itafungwa mapato hadi asilimia 40 yatapotea.
“Tunatarajia hiyo asilimia 40 ifikie asilimia 67, mkataba wa ukodishaji utahusisha gati namba 4,5 6 na 7 kati ya magati 12 yaliyopo bandarini,”amesema.
Aidha amefafanua kuwa bandari ya Dar es Salaam ni hazina kubwa kwa nchi na ndiyo maana serikali imetoa kipaumbele ambapo asilimia kubwa ya mizigo inayotoka kwenye nchi zilizopakana na Tanzania haipiti kwenye bandari ya Dar es Salaam.
Amesema Tanzania inapakana na nchi 8 ambazo hazina bandari lakini huduma inayozihudumia ni kidogo.
Amesema katika ujenzi wa bandari kutajengwa bandari kavu ambazo zitajengwa zitapunguza makontena katika bandari na changamoto katika barabara.
Katika hatua nyinmgine, Matinyi amesema Idara hiyo imeandaa programu maalum ya taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo Mikoani.
Amesema program hiyo itazinduliwa Jijini Dodoma Nov 01,2023, itakayowapa nafasi Wakuu wa Mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri zao kuwaeleza Wananchi wao ni nini Serikali imefanya katika Mkoa.
“Idara ya Habari (MAELEZO) imeandaa programu maalum ya taarifa ya maendeleo ya miradi Mikoani, na programu hii tunakwenda kuizindua Jumatano November 01,2023 Mkoani Dodoma, November 02 tutakuwa Morogoro, November 03 Pwani na November 04 Dar es salaam.
“Ni programu itakayowapa nafasi Wakuu wa Mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri zao kuwaeleza Wananchi wao ni nini Serikali imefanya katika Mkoa.
“Kwahiyo tutafika katika Mkoa tutamwita Mkuu wa Mkoa atakuja na Wakuu wake wa Wilaya lakini tunataka tuwape nafasi Wakurugenzi kwasababu tunataka kusikia habari za utekelezaji,”amesema.
Matinyi amefafanua kuwa “Katika muundo wetu fedha zinapelekwa kwenye Halmashauri kule ndio utekelezaji unakwenda ukisikia Shule, Hospitali imejengwa ni Afisa Elimu, Mtu wa Afya, Mhandisi, Boss wao nani? Mkurugenzi hii ndio sababu tumewachagua Wakurugenzi, sio kama tumemruka Kiongozi mwingine, tunataka Watanzania wajue Serikali inafanya nini kwenye Halmashauri, Serikali inafanya mambo mengi ila Wananchi hawana habari,”alisema.
Amesema wanatarajia baada ya hapo kuwa na vipindi vya habari vitakavyokuwa vinarusha habari za maendeleo ambapo kundi la pili litaanza Novemba, 2023 litahusisha mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga.
Amesema serikali imekuwa ikitekeleza miradi mingi ambayo wananchi hawaifahamu hivyo ni wakati sasa wa kujua nini kinafanyika katika Mikoa.