Kaimu Rasi wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam Dkt. Coretha Komba (kushoto) akimkabidhi cheti mhitimu wa mafunzo ya jinsi ya kutumia maktaba katika kutafuta taarifa kwa njia ya kisasa kwa ajili ya kufanya tafiti (Library and Bibliographic Research Skills) Mkutubi wa Wizara ya Kilimo Bi. Victoria Shirima wakati akifunga mafunzo hayo Jijini Dar es Salaam.
Kaimu Rasi wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam Dkt. Coretha Komba akizungumza na wahitimu wa mafunzo ya jinsi ya kutumia maktaba katika kutafuta taarifa kwa njia ya kisasa kwa ajili ya tafiti (Library and Bibliographic Research Skills) wakati akifunga mafunzo hayo Jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Kitengo Cha Maktaba Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam Bw. Elias Ntobi akifafanua jambo wakati akifundisha mafunzo ya Library and Bibliographic Research Skills.
Mratibu wa Mafunzo Bw. Bernard Msengi akifafanua jambo wakati akifundisha mafunzo ya Library and Bibliographic Research Skills.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo wakiwa darasani.
Baadhi ya wahitimu wakipokea vyeti
Kaimu Rasi wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam Dkt. Coretha Komba akiwa katika picha ya pamoja na wahitimu wa mafunzo ya Library and Bibliographic Research Skills.
……..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam imewajengea uwezo wadau kutoka Taasisi mbalimbali za elimu ya juu ili kujua jinsi ya kutumia maktaba katika kutafuta taarifa kwa njia ya kisasa (Library and Bibliographic Research Skills) kwa ajili ya matumizi ya kufanya tafiti ambazo ni muhimu katika kulisaidia Taifa.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam wakati akifunga mafunzo ya kuwajengea uwezo jinsi ya kutumia maktaba kupata taarifa kwa ajili ya kufanya tafiti, Kaimu Rasi wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam Dkt. Coretha Komba, amesema kuwa mafunzo hayo yamefanyika kwa muda wa wiki moja ambayo yanakwenda kuwa msaada kwa watafiti hasa wakati wa kutafuta taarifa katika maktaba kwa ajili ya kufanya tafiti.
Dkt. Komba amesema wakati umefika wa kutumia vizuri maktaba katika kutafuta vyanzo mbalimbali vya taarifa ambavyo vitawasaidia kufikia malengo katika kufanya tafiti yenye ubora na kuleta tija kwa Taifa.
Amesema kuwa katika utekelezaji wa kufanya tafiti lazima uanzie katika maktaba kwa ajili ya kupata taarifa kutoka vyanzo mbalimbali.
“Maktaba ni sehemu muhimu kwa mtu ambaye anataka kufanya tafiti, hivyo tunatoa mafunzo hayo kwa ajili kuwajengea uwezo namna kutumia maktaba wakati wa kutafuta taarifa kwa ajili ya kufanya utafiti” amesema Dkt. Komba.
Amewakaribisha watu wote kushiriki katika mafunzo mbalimbali katika Chuo Kikuu Mzumbe ikiwemo namna ya kutumia maktaba katika kufanya tafiti, kwani ni muhimu kwa mtu au Taasisi yoyote ambayo inafanya kazi ya kuandaa tafiti.
Mkuu wa Maktaba Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam Bw. Elias Ntobi, amesema kuwa mafunzo hayo yanakwenda kuwasaidia washiriki katika kuhakikisha wanakuwa msaada katika taasisi wanazofanyia kazi.
Bw. Ntobi amesema kuwa wametoa elimu ya jinsi ya kutafuta taarifa kwa sababu duniani kuna machapisho mengi, hivyo ni muhimu kujua machapisho gani ambayo yanaweza kusaidia katika kujua taarifa fulani kwa ajili ya kufanya tafiti.
“Unapofanya tafiti unatafuta fact, ukifanya tafiti unapata majibu ya matatizo mbalimbali na kuisaidia Taifa” amesema Ntobi.
Nao baadhi ya washiriki wamesema kuwa mafunzo hayo yamewasaidia kwa asilimia kubwa katika kutafuta taarifa mbalimbali kwa njia ya kisasa katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mkutubi wa Wizara ya Kilimo Bi. Victoria Shirima, amesema kuwa wateja pamoja watumiaji wa maktaba watakwenda kupata taarifa mbalimbali kwa wakati ambazo zitawasaidia katika kufanya tafiti na kufikia malengo tarajiwa.
“Nimejifunza vitu vingi katika digital ambapo sasa nakwenda kuisaidia taasisi yangu kutafuta taarifa kwa ajili kufanya tafiti katika mada fulani ambayo imekusudiwa” amesema.