Na. Brigitha Kimario- TANAPA, Arusha
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki amelipongeza Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa utendaji kazi wake, na kusisitiza kuendelea kufuata taratibu, sheria, sera na miongozo ili kuleta tija na ufanisi katika utendaji kazi wa kila siku.
Ameyasema hayo leo tarehe 28.11.2023 akiwa katika ziara ya kikazi katika Ofisi za Makao Makuu ya Shirika hilo jijini Arusha.
“Niwapongeze sana kwa jitihada mnazozifanya katika ulinzi, uhifadhi na namna mnavyo simamia shirika, muendelee kufuata miongozo mliyojiwekea bila kusahau kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, sera, taratibu na miongozo mbalimbali inayotolewa na wakuu wa nchi.”
Aidha, katika kutatua migogoro kati ya Hifadhi za Taifa na wananchi waishio jirani ameitaka TANAPA kuendelea kuzuia uvamizi kwenye maeneo ya hifadhi na kutatua migogoro iliyopo kwa kuzingatia sheria.
“Endeleeni kuzuia uvamizi katika maeneo ya hifadhi na wale wanaopaswa kuondolewa basi fuateni sheria, taratibu na haki za binadamu ili kuepuka migongano na wananchi. ” alisema Waziri Kairuki.
Vilevile, ameisisitiza menejimenti ya TANAPA kusimamia rasilimali watu vizuri na kupatiwa mafunzo ili kuwaongezea weledi huku akiwataka watumishi kila mmoja kuonesha uwezo wake ili kuleta ufanisi katika shughuli za kila siku.
” Nawapongeza kwa kuongeza mapato pamoja na hayo menejimenti endeleeni kutengeneza fursa za watumishi kupata mafunzo ya kila mara ili kuendana na ukuaji wa teknolojia.”
Naye, Kaimu Kamishna wa Uhifadhi – TANAPA Juma Kuji amemshukuru Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki kwa ujio wake na kuahidi kufuata maelekezo yote aliyoyatoa na hatimae kufikia lengo la watalii milioni tano ifikapo mwaka 2025.
” Tumepokea maelekezo yako na tumejipanga kuongeza watalii zaidi kwa kuimarisha miundombinu ya barabara, kuongeza sehemu za malazi na kuhamasisha wawekezaji kujitokeza kuwekeza katika Hifadhi za Taifa, ili tufikie watalii milioni tano ifikapo 2025.”
Hii ni ziara ya kwanza kwa Waziri Kairuki katika ofisi za Makao Makuu ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) tangu alipoteuliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.