Na Sophia Kingimali.
Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalumu imeitaka sekta binafsi kushirikiana katika kuwainua wamachinga ili waweze kuondokana na changamoto mbalimbali walizonazo hasa mitaji.
Akizungumza kwa niaba ya waziri wa maendeleo ya jamii leo Oktoba 28, 2023 kwenye kongamano la wamachanga liliandaliwa na taasisi ya Hatua kwa Hatua na Mama pamoja na taasisi ya Vijana Imara Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt Anandele Mhando amesema taasisi za fedha zinapaswa kuangalia kiwango cha riba kwenye mikopo ya wamachinga ili waweze kuwasaidia kuinua biashara zao.
“Taasisi za fedha tuziombe na kuzipongeza ambazo tayari zinawasaidia mikopo ya riba nafuu wamachinga waendelee kufanya hivyo ikiwezekana kupunguza riba kabisa ili tuweze kuwasaidia hawa wamachinga waweze kuwa wafanyabiashara wakubwa”amesema Dkt. Mhando
Aidha amewataka wakurugenzi kuhakikisha wanawashirikisha wamachinga kwenye ujenzi wa masoko na miundombinu ya masoko.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Saad Mtambule amezitaka ofisi zote za wilaya na manispaa kuendelea kuwaunga mkono wamachinga kwenye shughuli zao kwa kuwapunguzia usumbufu wanaokutana nao.
Amesema wilaya ya Kinondoni inamasoko 28 ambapo serikali imetoa pesa ya kuboresha miundombinu ikiwa ni pamoja na kujenga masoko mengine manne.
Aidha ameongeza kuwa serikali katika kuboresha mazingira kwa wafanyabiashara wadogo wameendelea kutoa mikopo.
“Serikali imeendele kujali wafanyabiashara wadogo imekuwa ikitoa mikopo kwa wajasiliamali mpango huo ambao umesimama tu kidogo kwa ajili ta kuboresha utoaji wa mikopo mara utaratibu utakapokamilika pesa hizo zitaendelea kutolewa kama kawaida”amesema
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wamachinga Mkoa wa Dar es salaam Namoto Namoto ameipongeza serikali kwa juhudi kubwa wanazozifanya katika kuwasaidia wamachinga.
Ameongeza kuwa wamekua na mradi wa kuwatafutia wamachinga ardhi ili nao waweze kukopesheka na mpaka sasa wameshapata ekari 130 Bagamoyo na ekari 75 wilaya ya ilala.
“Tunafanya hivi ili kuwafanya hawa wamachinga kukua na kuweza kukopesheka tunaamini wanapokuwa wafanyabiashara wakubwa watatoa ajira nyingi lakini pia kodi zitaongezeka kwa serikali”amesema Namoto.
Aidha ametoa wito kwa serikali kuwashirikisha wamachinga kwenye ujenzi wa masoko kwani wao ndio wahusika wakuu wa masoko hayo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Hatua kwa Hatua na Mama Bw. Amur Seif amesema kwa kutambua juhudi za Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa wamachanga ameamua kuandaa kongamano hilo kama hatua ya kumuunga mkono kwa juhudi zake za kuwaletea maendeleo wamachinga
“Hii hatua kwa hatua na mama imeona juhudi za Rais kwa wamachinga ikiwemo kuweka mazingira mazuri hasa katika upatikaji wa mikopo lakini pia kuboresha masoko ambayo ndio sehemu muhimu ya wamachinga kupata kipato chao”amesema
Sambamba na hayo Amur amewataka wamachanga kuchangamkia fursa ya kanzi data kwani itawasaidia kutambulika na kusaidiwa kwa wakati.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Vijana Imara Antu Mandoza amewataka wamachinga kuwa wabunifu kuendana na teknolojia ili kuwafikia wateja kwa haraka na kwa gharama Ile Ile.
Aidha Mandoza pia ameziomba mamlaka husika kufikiria minada ifanyike mpaka usiku ili kuwasaidia wamachinga kupanua wigo wa masoko yao kwa kuwahudumia mpaka wale wanaotoka kazini usiku.