Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango pamoja na Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga wakitembelea Mabanda ya Maonesho ya Wajasiliamali katika Viwanja vya Sababa Mkoani Njombe tarehe 28 Oktoba, 2023
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akizungumza na Wananchi wakati wa Hafla ya Kuhitimisha Maonesho ya SIDO katika Viwanja vya Sabasaba tarehe 28 Oktoba, 2023
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akisalimiana na Wananchi katika Viwanja vya Maonesho Sabasaba Mkoani Njombe tarehe 28,Oktoba 2023
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe akizungumza na Wananchi waliohudhuria hafla ya Kuhitimisha Maonesho ya nne ya SIDO Mkoani Njombe tarehe 28 Oktoba, 2023.
…………………………
*Tanzania kuwa nchi ya Kipato cha Kati.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango leo tarehe 28 Oktoba, 2023 amehitimisha rasmi Maonesho ya Shirika la Viwanda vidogo vidogo (SIDO) yaliyofanyika katika Viwanja vya Sabasaba katika Halmashauri ya Mji wa Njombe, Mkoani Njombe.
Dkt. Philip Mpango aliwasili viwanjani hapo na kuanza kutembelea mabanda mbali mbali ya maonesho ya bidhaa za Wajasiliamali hao na kujionea ubunifu tofauti katika Sekta ya Viwanda hapa nchini.
” Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano tunaoutekeleza hivi sasa unatutaka tukuze mchango wa Uchumi pamoja na Ajira zinazotokana na Viwanda katika pato la Taifa. Hivi sasa mchango wa Sekta ya Viwanda ni asilimia 7.1 tunatamani tufikie asilimia 9 ifikapo mwaka 2025 hadi 2026″. Amesema Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango amesisitiza kuwa, tafiti zina umuhimu mkubwa sana katika kukuza matumizi ya teknolojia mbali mbali kwenye Uzalishaji na uongezaji thamani wa bidhaa na mazao.
Katika Maonesho hayo ambayo Tume ya Madini ilishiriki, akizungumza mara baada ya kutembelea banda la Tume ya Madini. Dkt. Mpango amewataka Watendaji wa Tume ya madini kufanya utafiti ili kujua madini yapi yanapatikana eneo gani? na kuhakikisha takwimu mbali mbali zinapatikana hapa nchini ili kuongeza Pato la Taifa.
Dkt. Mpango amesema kuwa, maonesho ya SIDO yameshirikisha Wajasiliamali 628 na teknolojia 95 ambazo zinatumika kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao mbali mbali ikiwemo Parachichi linalozalishwa kwa wingi Mkoani Njombe.
Aidha, Dkt Mpango ameelezea kufurahishwa kwake na kauli mbiu ya Maonesho hayo ambayo inasema “kwa Pamoja tujenge Viwanda kwa Uchumi na Ajira endelevu” na kusema, Kauli hii iwahamasishe watu wote hasa vijana kuingia kwenye Sekta ya Kilimo, Viwanda na Biashara.
Akizungumza katika Maonesho hayo, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe amesema, Maonesho ya nne ya Wajasiliamali yamekuwa na ongezeko kubwa la washiriki ambapo mwaka 2018 walihudhuria Wajasiliamali 582 yalipofanyika kwa mara ya kwanza Mkoani Simiyu na mwaka 2023 idadi ya washiriki imeongezeka kufikia Washiriki 628.
Hafla ya kilele cha Maonesho hayo ambayo yamefikia tamati tarehe 28 Oktoba, 2023, yamehudhuriwa na Viongozi mbali mbali wa Serikali, Sekta Binafsi, Viongozi wa dini, Wajasiliamali pamoja na Wananchi.