Viongozi wa UWT Mkoa wa Magharibi Kichama wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa kamati ya habari na mawasiliano ya ziara ya Mwenyekiti wa UWT Tanzania,Marry Pius Chatanda inayotarajiwa kufanyika oktoba 29 mkoani humo.PICHA NA FAUZIA MUSSA –MAELEZO ZANZIBAR.
Na Fauzia Mussa, Maelezo
Uongozi wa Umoja wa Wanawake Tanzania Mkoa wa Magharibi kichama umempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kutekeleza vyema ilani ya chama cha Mapinduzi katika kipindi cha miaka mitatu.
Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi Mjumbe wa kamati ya utekelezaji UWT Mkoa wa Magharibi Mziwanda Ibrahim Abdalla amesema utekelezaji huo haukua wa maneno bali unaendelea kuonekana kwa vitendo.
Alisema mambo aliyoyafanya Rais huyo katika kipindi kifupi ni ya kupongezwa na kupigiwa mfano kutokana na kupindukia malengo.
Aidha alisema katika kipindi cha miaka 3 ya Dkt Mwinyi Serikali imefanikiwa kuleta mabadiliko makubwa Nchini ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya skuli za ghorofa, kuboreshwa kwa masoko,kuanzishwa kwa Hospitali za Wilaya na Mkoa zenye vifaa vinavyokidhi haja ya matibabu kwa Wananchi pamoja na kuongezeka kwa miundombinu ya barabara za ndani kwa kiwango cha lami.
“Yalikua mabati, sasa ndani ya mabati kumechomoza Spitali,maskuli na masoko”alifafanua Mjumbe huyo.
Amesema Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT ) utaendelea kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi zinazoonekana waziwazi za kuwaletea maendeleo Wananchi wake na kuahidi kuwarejesha tena madarakani ifikapo 2025.
“Tulikua tunaona tu gari zinapita juu,Mpaka Tanzania bara gari zinapita juu,sasa tunaenda kuona kwa macho yetu dalili zimeanza kuonekana Mwanakwerekwe pale”alisema Mjumbe huyo.
Wakati huohuo Mjumbe huyo alitumia fursa hiyo kuwaomba wanachama,na wapenzi wa chama cha mapinduzi kuhudhuria katika mkutano wa hadhara unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu katika viwanja vya Mzee Mgeni Mambosasa mara baada ya kukamilika kwa ziara ya Mwenyekiti wao Taifa katika Mkoa huo.