Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Burhan (wa tatu kushoto) akipokea mfano wa hundi ya zaidi ya Tsh 374 milioni, kutoka kwa Mkuu wa Idara ya Kilimo Biashara wa NMB, Nsolo Mlozi (watatu kulia) kwa ajili ya fidia ya wakulima wa tumbaku walioharibiwa mazao yao na mvua kwa msimu wa 2022/2023 kwenye hafla iliyofanyika mkoani Tabora. Wanaoshuhudia ni Meneja wa Mamlaka ya Bima kanda ya Magharibi Dkt. Lupilya Emmanuel (wa pili kushoto), Afisa Mkuu wa Fedha wa kampuni ya Bima ya UAP, Nelson Rwihula(wa pili kulia) na Mkuu wa Idara ya Bima Benki ya NMB, Martine Massawe.
Benki ya NMB imesaidia wakulima wa tumbaku zaidi ya 400 mkoani Tabora kulipwa kwa wakati fidia ya hasara waliyopata baada ya mashamba yao kuharibiwa na mvua kubwa za mawe msimu wa 2022/2023. Hundi ya malipo ya madai hayo ya kiasi cha zaidi ya Shilingi milioni 374 kutoka kampuni ya bima ya UAP, imekabidhiwa kwa Mkuu wa Mkoa huo, Balozi Dkt. Batilda Burhani, aliyesema kuwa fidia hizo ni kubwa kuwahi kulipwa wakulima wengi nchini kwa wakati mmoja.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya mfano wa hundi wa kiasi hicho cha fedha, Dkt Batilda alieleza kuwa ushiriki wa NMB katika kulikamilisha hili kwa haraka kunaifanya kuwa zaidi ya benki katika kulihudumia taifa, lakini pia kuendana na azma ya serikali kuhakikisha wakulima wote nchini wana bima.
Kiongozi huyo aliongeza kuwa, wakulima waliokatia mashamba yao bima dhidi ya majanga walifanya maamuzi sahihi, kwani bima hizo zimekuwa mkombozi wao na sasa wataweza kuendelea na shughuli zao wakiwa na uhakika. Alizishukuru Benki ya NMB na UAP kwa juhudi za kuhakikisha fidia hii inalipwa kwa haraka si tu zinafanya waathirika kuendelea na kilimo chao, lakini pia zinawapa imani na bima na kuwaonyesha umuhimu wa kuwa na kinga dhidi ya majanga hasa kubima na NMB.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitendo cha Kilimo Biashara wa benki hiyo, Bw. Nsolo Mlozi, amesema Benki ya NMB inaunga mkono juhudi za Serilaki kuhakikisha kilimo nchini kinakuwa na tija na kuwanufaisha wakulima. Hivyo wskishirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Bima (TIRA) wataendelea kuhakikisha wakulima wengi wanapata elimu kuhusu Bima kwani majanga hayatabiriki.
Aidha, alisema mara tu baada ya wakulima hao kufikwa na madhira hayo, Benki ya NMB na Kampuni ya UAP walifanya upembuzi stahiki na tathmini ya kina kuona ni fidia kiasi gani inastahili kwa uharibifu wa mashamba husika na leo wamekabidhi malipo hayo.
Mwakilishi wa UAP, Bi Mariam Hussein, alisema kuwa lengo la kushirikiana na NMB ni kuhakikisha kuwa huduma za bima zinachangia kikamilifu kuendeleza kilimo na kuleta maendeleo ya uchumi nchini. Aliwaasa wakulima ambao hawajakata bima, kutembelea matawi ya NMB nchi nzima kukata bima.