Na Selemani Msuya
MWENYEKITI wa Kamati ya Mambo ya Nje ya Baraza la Mashauriano la Kisiasa la Watu wa China (CPPC), He Ping kesho atakuja nchini Tanzania akiwa ameambatana na wenzake watano.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.
Butiku amesema Ping na wenzake watano wanakuja kwa mwaliko wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere baada ya kuomba wawaalike, ombi ambalo limekubaliwa na serikali pia.
Amewataja wanaoambatana na Ping ni pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje, Wang Bingnam, Wajumbe wa Kamati, Hu Shishe, Kong Moi, Yang Xinwei na Xiao Oian.
“Kesho tuna ugeni mkubwa wa viongozi wa Chama cha Kikomunisti cha China, ambao tumewaalika na watatembelea MNF Oktoba 27,2023, ambapo tutazungumza mambo mengi yenye kujenga ushirikiano kati ya Tanzania na China,” amesema.
Mwenyekiti huyo amesema pia ugeni huo utaenda kuonana na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa William Anangisye, pia watatembelea Maktaba ya UDSM, Kituo cha Confusion na Makumbusho ya Taifa.
Butiku alisema MNF imekuwa ikishirikiana na China kwa muda mrefu tangu wakati wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere na kwamba wao watahakikisha wanaendeleza ushirikiano huo.
Amesema yeye amekuwa akitumiwa na China kama mshauri wa kitaalamu kupitia Chuo cha Zejiang cha huko China, hivyo mchango wao kwa nchi hiyo bado unaendelea.
Amesema wageni hao pia ambao wamebobea katika masuala ya habari watakuwa na mambo mengi ya kujifunza kupitia ziara hiyo.
Mwenyekiti huyo amesema wao kama taasisi wataendelea kuboresha ushirikiano na China hasa kipindi hiki ambacho taifa hilo linapambana kuzipigania nchi zote hasa zinazoendelea kuwa na uchumi imara.
“Nadhani mmeona kwa sasa China kupitia Belt and Road Initiative (BRI), inaonesha ilivyodhamiria kuinua nchi zinazoendelea, hivyo ujio huu ni mwendelezo wa dhamira yao,” amesema.