Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea taarifa ya timu aliyoiteua ya kuchunguza tuhuma za ubadhirifu wa fedha kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji kutoka kwa Mwenyekiti wa timu hiyo, Shedrack Kimaro, ofisini kwa Waziri Mkuu Mlimwa jijini Dodoma, Oktoba 25, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza baada ya kupokea taarifa ya timu aliyoiteua ya kuchunguza tuhuma za ubadhirifu wa fedha kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, ofisini kwa Waziri Mkuu Mlimwa jijini Dodoma, Oktoba 25, 2023. Kulia kwake ni Naibu Waziri wa TAMISEMI, Deogratius Ndejembi na kushoto kwake ni Mwenyekiti wa timu hiyo, Shedrack Kimaro. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
………..
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea taarifa ya uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa fedha kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji ambapo imebainika watu 10 wanahusika na mtandao wa uhamishaji fedha kinyume cha taratibu.
“Taarifa nimeipokea na mapendekezo ya Kamati wote tumeyasikia. Hatua za haraka zichukuliwe kwa sababu Mheshimiwa Rais anatafuta fedha za kuleta maendeleo lakini kuna watu wachache wanafanya ubadhirifu,” amesema.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo leo (Jumatano, Oktoba 25, 2023) ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma, Waziri Mkuu amesema kila mtumishi wa umma ni lazima atunze na kuratibu vizuri matumizi ya fedha zinazopatikana.
Amewataka Mawaziri na Makatibu Wakuu wasiridhishwe na taarifa za miradi wanazopokea pindi wakiwa ziarani kwani licha ya kuwa kuna wataalamu wanatoa taarifa nzuri mbele ya viongozi hao, bado kuna tricks wanachezacheza.
Akiwa kwenye ziara ya kikazi mkoani Kigoma, Septemba 20-22, mwaka huu, Waziri Mkuu alipata taarifa ya uwepo wa fedha zilizoingizwa kwenye akaunti ya Amana ya Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji kutoka TAMISEMI na kisha fedha hizo kuondolewa baada ya muda bila maelekezo maalum wala kujua zilitumikaje.
“Hapa Manispaa mnapokea fedha, zinakaa kwenye akaunti kwa muda halafu zinapotea, hazijulikani zimefanya nini. Nitaleta timu, waje wafuatilie hapa Kigoma, waende hadi TAMISEMI ili tuone huo mnyororo unaenda wapi,” alisema Waziri Mkuu wakati akizungumza na viongozi wa dini, Serikali, Chama cha Mapinduzi (CCM) na watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma na Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma kwenye ukumbi wa NSSF, Kigoma mjini Septemba 22, mwaka huu.
Mapema, akitoa taarifa kwa niaba ya wenzake, Mwenyekiti wa timu ya uchunguzi, alisema timu hiyo ilibaini kuwa uchepushaji wa fedha hizo unafanyika kwa kutumia njia kadhaa ikiwemo kuomba kibali kutoka HAZINA cha kuvuka na bakaa ya fedha za miradi mwaka wa fedha unapokaribia kwisha.
“Timu ya uchunguzi imebaini kuwa jumla ya sh. milioni 463.59 zilitumwa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma na hazikuwa kwenye mpango wala bajeti ya Manispaa na hazijawahi kuombewa matumizi kama bajeti ya ziada,” alisema.
Aliwataja watumishi waliohusika na uchepushaji wa fedha hizo kuwa ni Bw. Ferdinand Simon Filimbi, Bw. Salum Juma Said, Bw. Kombe Salum Kabichi, Bw. Athumani Francis Msabila, Bw. Moses Charles Zahuye, Bi. Jema Linus Mbilinyi, Mhandisi Joel Langford Shirima, Bw. Aidan Zabron Mponzi, Bi. Tumsifu Christopher Kachira na Bw. Mzee Mohamed Ubwa. Alisema watumishi hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote.
Alisema mbali ya watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma, wamo pia maafisa kutoka TAMISEMI, HAZINA na baadhi ya wafanyabiashara ambao wanatumiwa ili kupitisha miamala ya fedha hizo.
Wakati huohuo, Mwenyekiti huyo alisema kuna ubadhirifu mkubwa unafanyika kupitia Kitengo cha Usimamizi wa Fedha katika Akaunti Jumuifu ya Amana kilichopo TAMISEMI. “Timu imebaini kuwa Kitengo cha Usimamizi wa Fedha katika Akaunti Jumuifu ya Amana kilichopo TAMISEMI kinahusika kutuma fedha kwenye Halmashauri mbalimbali na kisha kuzitoa kwa kushirikiana na watumishi wa Halmashauri hizo.”
Alisema baadhi ya Halmashauri zinakuwa hazijaomba kibali cha kuvuka na fedha za bakaa kutoka HAZINA lakini zinatumiwa fedha hizo, kuna ambazo zinaomba kibali lakini zinapewa pungufu ya fedha zilizoomba na zinazobakia hazijulikani zinafanya nini.