Na.Sophia Kingimali
Serikali imewahakikishia wawekezaji katika Sekta ya Madini nchini kuwa itaendelea kuweka mazingira rafiki na wezeshi katika mnyororo mzima wa thamani katika Sekta ya Madini kama Sera ya Madini ya Mwaka 2009 inavyoelekeza.
Hayo ameyasema leo Oktoba 25, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt.Doto Biteko wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan katika Ufunguzi wa Jukwaa la Madini na Uwekezaji Tanzania 2023 jijini Dar es salaam lenye kauli mbiu inayosema ” Kuifungua Tanzania katika Fursa za Uwepo wa Madini”
Ameongeza kuwa kwasasa Serikali ina mpango wa kufanya utafiti wa kina wa jiofizikia katika eneo lote la nchi ili kupata taarifa za aina ya miamba na madini yaliyopo ili kuwepo na Kanzidata ya taarifa itakayosaidia katika utafiti wa kina.
Dkt.Biteko amefafanua kuwa kuwepo kwa taarifa za utafiti kutawezesha kufungua migodi zaidi pamoja na kuongeza kasi ya kukua kwa uchumi kwa kufungamanisha sekta ya madini na sekta nyingine za kiuchumi kama vile Maji na Kilimo.
Akielezea kuhusu uboreshaji wa miundombinu katika migodi mikubwa na midogo Dkt.Biteko ameeleza kuwa tayari mitambo mitano ya Uchorongaji miamba kwa wachimbaji wadogo imekabidhiwa na ifikapo mwezi juni 2024 mitambo mingine kumi itakabidhiwa.
Dkt.Biteko ameongeza kuwa mpaka sasa zaidi ya migodi 360 ya wachimbaji wadogo imeunganishwa na Nishati ya Umeme pamoja na kampuni kubwa 9 za zimeingia ubia na Serikali katika utafiti na uchimbaji madini ya kimkakati yakiwemo madini ya Nikeli, Kinywe , Makaa ya Mawe.
Awali , Waziri wa Madini Anthony Mavunde ameeleza kuwa Mkutano huu wa mwaka 2023 unatoa fursa kwa kampuni za madini kujadili kuhusu taarifa za namna ya upatikanaji wa mitaji , Utafiti , Uchimbaji na Uchenjuaji na uwekezaji kwa kuzingatia mazingira rafiki baina ya Serikali na Taasisi na Kampuni binafsi.
Akizungumzia kuhusu umuhimu wa taarifa za jiolojia Mavunde amesema uwepo wa taarifa za utafiti wa jiolojia na Jiofizikia kutawezesha kujua aina ya mashapo yaliyopo na kuchimba kwa uhakika na kuwepo kwa uwekezaji wenye uwiano sawa baina ya Serikali na Wadau wa Sekta ya Madini hasa katika uvunaji madini kibiashara.
Kwa upande wake Waziri wa Madini nchini Malawi Monica Changanamuno amesema kuwa anaamini kupitia jukwaa hili atajifunza mengi juu ya mipango ya maendeleo ya sekta ya madini nchini Tanzania hasa kwenye madini ya Kimkakati na madini adimu.
Aidha , akielezea kuhusu mikakati ya Serikali ya Malawi kupitia Vision ya 2036 , ameeleza kuwa Serikali ya Malawi imefanikiwa kufanya utafiti wa Jiolojia kwa asilimia 80 na kugundua madini mbalimbali yakiwemo madini kimkakati na madini adimu ( Rare Earth Elements) ambayo yote yapo katika mpago wa uwekezaji.
Akielezea kuhusu utafiti wa kina Waziri wa Madini wa Uganda Peter lokeris amesema jiolojia ya Afrika inatofautiana kidogo hivyo ni muhimu kufanya utafiti wa kina ili kubaini wingi na ubora wa madini yaliyopo katika sehemu husika kuwepo kwa taarifa za namna hiyo kutarahisisha kuvutia wawekezaji bila kuhangaika na upembuzi yakinifu.
Akielezea mkakati wa sekta ya madini nchini Uganda Waziri lokeris amesema kwasasa Serikali ya Uganda kwa kushirikiana na sekta binafsi inaendelea na ukusanya wa taarifa za kina kwenye Madini na Mafuta ili kupata sahihi za uwekezaji.
Aidha Waziri amezitaka Serikali za Afrika kuanza kufikiria kuzalisha Nishati umeme kupitia madini ya Uraniam kama Uganda ilivyoanza.
Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali akifungua Jukwaa ameeleza kuwa jukwaa hili ni sehemu ya Utekelezaji wa Sera ya Madini ya Mwaka 2009 yenye lengo la kuvutia uwekezaji katika Sekta ya Madini kwa kufanya majadiliano na kutoa mapendekezo ya namna gani ya kuboresha Sera ya Madini ya Mwaka 2009.
Akielezea maendeleo ya Sekta ya Madini , Mahimbali amefafanua kuwa Sekta imeendelea kukua ambapo kwasasa katika Pato la Taifa inachangia asilimia 9.1 kwa mwaka 2022.
Aidha sekta ya Madini kwa mwaka 2021 ilitoa ajira 14308 na Mwaka 2022 kiwango kiliongezeka mpaka kufikia 16462.
Sambamba na hapo kuna ongezeka la mauzo ya bidhaa zitokanazo na madini mfanokwa mwaka 2021 mauzo yalikuwa bilioni 3.1 kwa mwaka 2022 yameongezeka kufikia mwaka 3.4.