Waziri wa Nchi ofisi ya Rais TAMISEMI Mohamed Mchengerwa ametaka Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) maarufu kama mwendokasi kuongeza ufanisi pamoja na kuongeza ubunifu ili kutoa huduma bora ya usafiri kwa watanzania
Mchengerwa ameyasema hayo Leo Akiwa katika muendelezo wa ziara zake kukagua na Kupitia Kila idara iliyochini ya wizara yake ambapo Leo amekutana na watendaji wa DART na kuwataka watendaji hao kuwa wabunifu na kuacha kufanya kazi kwa mazoea na kuanza kubadilika katika ufanisi wa kazi ili kuboresha mradi huo ikiwemo kupunguza adha mbalimbali zinazowakabili watumiaji wa usafiri Huo.
Aidha waziri Mchengerwa amewataka watendaji wa DART kuangalia uwezekano wa kuongeza watoa huduma wengine wa usafiri huo ili kuongeza ushindani na ufanisi katika mradi huo hasa katika njia mpya zitakazoanza kutumika hivi karibuni.
Hata hivyo Waziri Mchengerwa ameagiza kutengenezwa kwa magari yote yaliyoharibika na kuandaa mpango wa kununua Mabasi yanayojitosheleza ili kupunguza msongamano wa abiria vituoni na kuwahi kwenye shughuli zao za kujiongezea kipato
Pia Waziri Mchengerwa amewataka uongozi wa DART kuimarisha mifumo ya kutoa Taarifa mara tu panapoteka changamoto yeyote ya usafiri.
“Sijapenda kuendelea kuona vurugu kwenye Vituo vya kusubiria mabasi, ni vyema panapotokea hitilafu kuwe na mifumo ya kutoa taarifa ili kupunguza manung’uniko kwa wananchi ambao huenda wamekaa pale muda mrefu kusubiria basi,”amesema.
Awali, akitoa taarifa za utendaji kazi wa Wakala huo, Mtendaji Mkuu wa DART, Dkt. Edwin Mhede amesema katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya Awamu ya sita, uwezo wa kusafirisha abiria kwa siku umeongezeka kutoka abiria 90,000 mpaka 210,000 na umetokana na maboresho makubwa yaliyofanyika kwa Wakala huo.