Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha inainua ustawi wa vijana kiuchumi.
Hayo yamesemwa leo Oktoba 24, 2023 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba ( Mb) katika Maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Mataifa katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.
Waziri Kairuki alisema njia mbalimbali zimekuwa zikitumika na serikali katika kuhakikisha kwamba vijana wanapiga hatua kiuchumi.
“Kwa upande wa Tanzania Bara, Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007 inafanyiwa mapitio ili kuakisi hali ya sasa ya maendeleo ya vijana, vipaumbele na changamoto” Mhe. Kairuki amesisitiza.
Ametaja moja ya mkakati ni kuwezesha vijana kupitia Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ambalo hutoa mikopo kwa vijana wajasiriamali na uanzishwaji wa zaidi ya mifuko 45 maalum katika wizara na idara mbalimbali ili kuhakikisha kuwa vijana wanawezeshwa kiuchumi.
Amefafanua kuwa Serikali ya Tanzania imehakikisha kuna ongezeko la upatikanaji wa huduma za ushauri nasaha rafiki kwa vijana kupitia programu ya Afya ya Ujinsia na Haki za Uzazi na kuongeza upatikanaji wa huduma za matunzo na matibabu ya VVU.
Amesema kupitia Mpango wa Kujenga Kesho Bora – YOUTH INITIATIVE FOR AGRIBUSINESS, Serikali inatarajia kuongeza ushiriki wa vijana katika sekta ya kilimo na kuharakisha kasi ya ukuaji wa sekta ya kilimo kwa ajili ya maisha endelevu na bora.
Kufuatia juhudi hizo, bado vijana wameendelea kukumbwa na changamoto mbalimbali hivyo, Mhe. Kairuki amezitaka jumuiya zote za Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa na Mashirika mengine ya Kikanda kuwa na nguvu ya pamoja ili kuweka sera na mikakati madhubuti ya kukabiliana na changamoto hizo.
Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki amewaasa vijana kuwa wabunifu na kutumia teknolojia ambayo ni nguzo muhimu za kukuza uwezeshaji wa vijana.
” Ni muhimu kusaidia wajasiriamali wachanga katika kubadilisha mawazo yao kuwa biashara zinazofaa, endelevu kupitia kujenga uwezo na upatikanaji wa masoko na matumizi ya teknolojia na uvumbuzi.” amesema.
Kaulimbiu ya Siku ya Umoja wa Mataifa ni;: Kuinua Idadi ya Vijana wa Tanzania”