NA MWANDISHI WETU, NJOMBE

Benki ya NMB imesema imeshirikiana na serikali kuhamasisha uwepo wa maonesho ya nne ya viwanda vidogo Sido mkoani Njombe.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa maonesho hayo viwanja vya sabasaba mjini Njombe meneja mahusiano mwandamizi huduma za 

benki kwa serikali Josephine Kulwa,amesema maonesho hayo ni fursa kwa wajasiriamali wadogo na wafanyabiashara mkoani Njombe kupata elimu ya mambo mbalimbali ikiwemo huduma zinazotolewa na benki ya NMB.

“Lengo la kudhamini kuhamasisha maonesho haya ni kutoa fursa kwa wajasiriamali,wakulima,wafanyabishara waweze kufahamu uwepo wa maonesho haya,benki ya NMB ambacho tumekuja nacho hapa kwanza tunatoa elimu ya ujasiriamali,tunatoa elimu ya kufedha na kukuwezesha kuona jinsi ganj unaweza kukopesheka na mabenki mbali mbali hasa kwa upande wa benki ya NMB tunafanya mikopo mbalimbali kwa wajasiriamali ikiwemo mkopo wa mshiko fasta”alisema Josephine.

Josephine alisema NMB imefarijika kuwa mdhamini mkuu wa maonesho hayo na kwamba wataendelea kushirikiana na serikali katika mambo mbalimbali.

Mgeni rasmi ambaye ni naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Exaud Kigahe,akizungumza wakati wa uzinduzi wa maonesho ya nne ya Sido kitaifa mkoani Njombe amewashukuru benki ya NMB kwa kuhakikisha maonesho hayo yanafana.

Aidha pia amewataka wananchi kutumia vizuri fursa ya maonesho ya SIDO ili kupata teknolojia itakayowawesha kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani mazao yao kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi.

Kigahe amesema serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa kwenye sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi hivyo ili kuunga mkono jitihada za serikali ni lazima teknolojia iendane sambamba na matarajio ya uwekezaji katika sekta ya kilimo ili kupata soko la uhakika. 

“Kilimo kiendane na kasi ya uongezaji wa thamani ili kudhibiti upotevu wa mazao, tuunganishe kilimo na viwanda itasaidia kupunguza uagizaji wa bidhaa nje na kuweza kuuza bidhaa zetu nje ya nchi badala yakuuza malighafi” Alisema Kigahe. 

Mkuu wa wilaya ya Njombe Mhe Kissa Kasongwa akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Njombe Antony Mtaka amewakaribisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza mkoani Njombe.

Awali Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Viwanda Vidogo Sido,mhandisu Prof Sylivester Mpanduji,alisema Sido imekuwa ikiwaunganisha wanaviwanda wadogo na wakati wenye uhitaji mkubwa wa mitaji katika taasisi mbalimbali za fedha.

Kauli mbiu ya maonesho hayo inasema “Pamoja tujenge Viwanda kwa uchumi na ajira endelevu” yameshirikisha wajasarimali zaidi 800 kutoka ndanina nje ya Tanzania.