Kamanda wa Polisi Mkoani Mbeya, Benjamin Kuzaga akionesha bunduki aina ya Gobore aliyokutwa nayo Mzee Pascal Mwango ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.(Picha na Joachim Nyambo).
…..
Na Joachim Nyambo, Mbeya.
MZEE mwenye umri wa miaka 80, Pascal Mwango mkazi wa Kijiji cha Madundasi Wilaya ya Mbarali Mkoani kwa tuhuma za kupatikana na bunduki aina ya Gobole bila kuwa na kibali cha umiliki halali.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Benjamin Kuzaga mzee huyo alikamatwa Oktoba 20 mwaka huu maeneo ya Masenjele ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha wakati Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Askari wa Jeshi la Uhifadhi – TANAPA likiwa katika misako na doria dhidi ya wawindaji haramu na majangiri wanaofanya uhalifu ndani ya hifadhi ya Taifa.
Aidha Kamanda Kuzaga amesema katika upekuzi mtuhumiwa alikutwa na bunduki moja aina ya gobole, risasi aina ya golori 35, unga wa baruti ukiwa kwenye mfuko wa plastiki, kisu kimoja, kiberiti kimoja na fataki mbili za kulipulia bila kibali cha umiliki halali wa vitu hivyo.
Amebainisha kuwa mtuhumiwa amekuwa akifanya uhalifu kwa kuwinda na kuua wanyama pori ndani ya hifadhi ya Taifa ya Ruaha kinyume cha sheria.
“Jeshi la Polisi lipo katika kampeni ya msamaha wa usalimishaji silaha haramu kwa hiari iliyoanza Septemba mosi na inatarajiwa kumalizika Oktoba 31, 2023.
Hivyo ni wito wa Jeshi la Polisi kwa wananchi wote wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kusalimisha kwa hiari katika vituo vya Polisi, ofisi za serikali za mitaa na ofisi za watendaji wa Kata.
Muda wa kusalimisha silaha ni kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa kumi jioni. Haujachelewa, salimisha silaha sasa katika kipindi cha msamaha.” Alihimiza Kamanda Kuzaga