Na Sophia Kingimali.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mohammed Abdulla, amesema Serikali inaendelea kuandaa mkakati wa uchumi wa kidigitali,kwa kuboresha mingozo ya kisera na kisheria, ili kuhakikisha nchi inakuwa na miundombinu itakayowezesha uwepo wa teknolojia mpya na za kisasa zinazoibukia.
Hayo ameyasema leo Oktoba 20, 2023, wakati akifunga kongamano la saba la TEHAMA2023 Jijini Dar es Salaam, ambapo amezitaka taasisi mbalimbaliu za Serikali na za binafsi, kuhakikisha wanafanya tafiti na kutoa elimu kwa jamii kuhusu teknolojia bora ya akili bandia ambazo zitaleta tija ya kiuchumi kwa kutoa ajira kwa vijana na makundi maalum.
“Wadau wote pamoja na serikali muendelee na ubunifu ili kukuza uchumi wa nchi yetu, pia taasisi zenye uwezo zitoe mitaji kwa kampuni za ubunifu za TEHAMA, ili zifanye vizuri zaidi katika ubunifu na kama nchi, iweze kufikia teknolojia ya kisasa ya kidigitali, aidha pia serikali na wadau imarisheni mawasiliano hasa vijijini” amesema Abdulla.
Aidha amezitaka pia taasisi za serikali kuhakikisha zinafuata miongozo na mifumo yote ya kutolea
huduma za kidigitali nchini, kwa kutumia namba jamii ambayo ni namba yakitambulisho cha Taifa (NIDA) na kusisitiza kuwa, namba hiyo itumike na wananchi wanapotaka kutumia huduma anayoitaka.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Selestine Kakele, amesema katika mkutano huo, mambo mengi ya muhimu yamejadiliwa ikiwepo kuwawezesha wanawake, vijana na walemavu katika TEHAMA, pamoja na kuunga mkono kampuni changa zilizoanzishwa na watu wa makundi hayo, kwa kuwapatia mafunzo na mitaji.
“Tanzania haina budi kuwa ni kitovu cha TEHAMA kwa kuunga mkono teknolojia inayochochea ubunifu, ili kujenga jamii yenye usawa katika uchumi wa kidigitali, Tanzania haina budi kuyawezesha makundi maalum hususan walemavu, tunaangalia uwezekano wa kuwa na siku au wiki maalum ya walemavu katika TEHAMA” amesema Bw. Kakele.
Nae Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA Dkt. Nkundwe Mwasaga amesema kongamano hilo limejadili mambo mengi ikiwepo mafanikio na changamoto zinazowagusa wanawake vijana na walemavu katika TEHAMA lengo likiwa ni kujenga uchumi wa kidigitali ambao ni jumuishi.