Na. Mwandishi Wetu, IJA
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher
Siyani amewataka Majaji wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania kuharakisha utoaji wa
hukumu ili wananchi wapate haki yao mapema.
Jaji Kiongozi ameyasema hayo jana tarehe 20 Oktoba, 2023 wakati
akifunga Mafunzo Elekezi ya wiki tatu
kwa Majaji wapya 20 wa Mahakama Kuu ya Tanzania katika Chuo cha Uongozi wa
Mahakama Lushoto (IJA), wilayani Lushoto mkoani Tanga.
Mafunzo hayo yaliandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa
kushirikiana na IJA, na yalifunguliwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim
Hamis Juma mnamo tarehe 02 Oktoba, 2023 hapa IJA Lushoto.
Mhe. Siyani amesema kuwa Mahakama ya Tanzania haitarajii
kuona Jaji au Hakimu anakaa na hukumu bila kuisoma kwa zaidi ya muda uliyowekwa
kisheria.
“Msizalishe viporo vya
hukumu wala
nakala za maamuzi yenu.
Dunia inakwenda kasi na watu
wanataka haki ipatikane kwa haraka. Hatutarajii, hatutarajii, hatutarajii kabisa kuwa Jaji au Hakimu, akae na
hukumu bila kuisoma kwa
zaidi
ya muda uliowekwa kisheria. Sambamba na kusoma hukumu zenu ni kutoa
nakala zake kwa wadaawa,”
amesema Mhe. Siyani.
Pia Mhe. Siyani amewahimiza Majaji hao kufanya kazi kwa
bidii kwani utamaduni wa sasa wa Mahakama ya Tanzania ni Majaji kufanya kazi
usiku na mchana ili kumaliza mashauri mapema.
“Moja kati
ya tamaduni iliyojengeka sasa hivi ni kufanya kazi
kwa bidii. Nawaambia kweli
tena bila
kupepesa macho, wengi
wa
Majaji wenzenu mnaoenda kujiunga
nao, hawalali.
Wanafanya kazi usiku na mchana. Mchana wanasikiliza mashauri na usiku wanaandaa maamuzi.
Jaji asiyeiga utamaduni huu, atatambulika haraka kuwa hachezi ngoma wanayocheza wenzake.
Ninyi mkaige utamaduni huu na mtapimwa sio tu na
Mahakama bali
na watanzania wenyewe,” amesisitiza Mhe. Jaji Kiongozi.
Aidha Jaji Kiongozi amewasihi Majaji hao kuwa wavumilivu
kwani watakutana na ukosoaji wa kila aina watakapokuwa wanatimiza wajibu wao wa
utoaji haki.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya washiriki wenzake, jaji
mpya wa Mahakama Kuu, Mhe. Dkt. Evaristo Longopa amesema kuwa mafunzo hayo yamewajengea
msingi ambao utawasaidia katika kazi yao mpya ya Ujaji wa Mahakama Kuu.
“Tunawashukuru wawezeshaji, wametupa ujuzi na mtazamo kuhusu
mambo mbalimbali ambayo yatatusaidia sana katika utendaji wetu wa kazi, tunaamini
mafunzo haya yametujengea msingi ambao utamsaidia kila mmoja wetu kutekeleza
majukumu yake kwa uadilifu na kwa ufanisi mkubwa,” amesema Mhe. Jaji Longopa.
Nao baadhi ya Washiriki wa Mafunzo hayo ambao ni Majaji wa
Mahakama Kuu, Mhe. Ntuli Mwakahesya na Mhe. Dkt. Dafina Ndumbaro wamebainisha
kuwa mafunzo hayo yamewawezesha kuzifahamu taratibu, sheria na utamaduni wa
Mahakama ya Tanzania na wameahidi kuyafanyia kazi kwa haraka mashauri kama
alivyosisitiza Mhe. Jaji Kiongozi.
Katika Mafunzo haya, Mada mbalimbali ziliwasilishwa na
wawezeshaji kutoka Mahakama ya Tanzania, Taasisi mbalimbali za Umma na za
binafsi.
Majaji hao wapya waliteuliwa na Mhe, Dkt. Samia Suluhu
Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo tarehe 3 Septemba, 2023 na
kuapishwa tarehe 14 Septemba, 2023 Ikulu jijini Dar es Salaam.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akitoa hotuba wakati akifunga Mafunzo Elekezi ya wiki tatu kwa Majaji wapya 20 wa Mahakama
Kuu ya Tanzania (hawapo pichani) katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto
(IJA), jana tarehe 20 Oktoba, 2023.
Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa
Mahakama Lushoto (IJA) Mhe. Dkt. Paul Kihwelo
akitoa neno kwa Majaji wapya wakati wa kufunga Mafunzo Elekezi ya wiki tatu yaliyofanyika katika
Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (aliyeketi mbele) akiwasilisha mada katika Mafunzo
Elekezi ya wiki tatu kwa Majaji wapya 20 wa Mahakama Kuu ya Tanzania katika
Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).
Jaji mpya wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Evaristo Longopa akitoa
neno la shukrani kwa niaba ya washiriki wenzake ambao ni Majaji wapya 20 wa
Mahakama Kuu ya Tanzania wakati wa ufungaji wa Mafunzo Elekezi ya wiki tatu kwa Majaji hao katika
Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani
(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Meza kuu wakati akifunga Mafunzo Elekezi
ya wiki tatu kwa Majaji hao wapya 20 wa Mahakama Kuu ya Tanzania katika Chuo
cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA). Wengine ni Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania na
Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) Mhe. Dkt. Paul Kihwelo (wa
pili kushoto), ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe.
Victoria Nongwa (wa pili kulia), Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe.
Awadh Mohamed (kwanza kushoto) na kwanza kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa
Mafunzo wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Patricia Ngungulu.
(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha – Mahakama)