Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, akiwasilisha Taarifa ya Utendaji wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu (haipo pichani) kwa kipindi cha Julai – Oktoba, 2023 Bungeni, jijini Dodoma.
Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Eng. Bernad Kavishe, akitoa maelezo kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso (hayupo pichani) wakati Kamati hiyo ilipokuwa ikipokea Taarifa ya Utendaji wa Bodi hiyo, jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mheshimiwa Selemani Kakoso, akifafanua jambo kwa wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu (hawapo pichani), wakati Kamati hiyo ilipokuwa ikipokea Taarifa ya Utendaji wa Bodi hiyo, jijini Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Mhandisi Aisha Amour, akitoa ufafanuzi wa hoja zilizowasilishwa na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, wakati Bodi ya Usajili ya Wahandisi (ERB), ilipowasilisha Taarifa ya Utendaji wa Bodi hyo, jijini Dodoma.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu wakisikiliza Taarifa ya Utendaji wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) iliyowasilishwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, jijini Dodoma.
…………
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Imewataka Bodi ya Usajili Wahandisi ( ERB) kuweza kusimamia miradi yao kwa ufanisi na kwa viwango vya hali ya juu.
Akizungumza mara baaada ya kupokea Taarifa ya kiutendaji ya Julai- Oktoba Bungeni, jijini Dodoma, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Selemani Kakoso, ameshauri Bodi kuwa na wataalamu wa kusimamia miradi ili ifanyike kwa umahiri na ufanisi zaidi.
“Tuangalie suala la ERB kuweza kusimamia miradi yote ambayo imepanga kuitekeleza kwa Wahandisi wazawa na wahandisi kutoka nje, mfano usimamizi wa Daraja la kutoka Serengeti hadi Tarime limejengwa na Wazawa na lipo vizuri sana”, amesema Mheshimiwa Kakoso.
Aidha, Mheshimiwa Kakoso ameongeza kuwa Wahandisi waunganishwe na Mafundi ili kuweza kufanya kazi kwa pamoja kwani italeta tija na hatimaye kuletea taasisi maendeleo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, ameishukuru Kamati ya kudumu ya Bunge la Miundombinu, na kusema kwamba Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, imewapa majukumu bodi hiyo kuweza kuwatambua kisheria Wahandisi wa chini ambao ni Wazawa.
“ Tumewataka ERB wawe na kanzidata ya kujua wahandisi wangapi waliopo Nje ya Nchi, na tunatambua ERB ni Taasisi kubwa ambayo ina wahandisi kila Sehemu ambao wanafanya kazi na Tanesco, Duwasa, REA hivyo kuwe na taarifa zao.
Naye, Msajili wa Bodi ya Usajili Wahandisi ( ERB) Mhandisi Bernad Kavishe amesema kuwa wamejipanga vizuri kuweza kuwainua wahandisi Wazawa katika kazi za miradi mbalimbali ambayo inatekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“ Tunaishukuru Serikali ya Awamu ya sita kwa kuendelea kuwaamini Wahandisi wetu wa ndani kwa kuweza kupata kazi ndani ya nchi ambazo wapo na wanafanya vizuri na kwa viwango, kazi ambazo zinafanywa ni pamoja na kusimamia Bwawa la Mwalimu Nyerere.
Pia ameongeza kuwa Wahandisi wengi wanapata ufadhili kupitia Serikali,na mafunzo ya muda mfupi yanatolewa na Bodi.Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu leo imepokea Taarifa ya Utendaji wa TBA kwa kipindi cha Julai – Oktoba 2023 iliyowasilishwa na Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo Mheshimiwa Innocent Bashungwa.