Na Mwamvua Mwinyi, Rufiji
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge ,ametembelea Maeneo yenye viashiria vya kutokea athari za Mvua za Elnino, ikiwemo eneo Mohoro na kuwaasa wakazi wa eneo hilo wahame.
Akizungumza na wananchi wa Muhoro Kunenge aliwataka ,kuzingatia maelekezo ya serikali ya kuhama eneo hilo kwani mwaka 2021 eneo hilo liliathirika na Mvua kubwa na Serikali kulazimika kutafuta eneo mbadala kwa ajili ya wananchi hao.
Alisema , Serikali imeona ianze kujipanga na kudhibiti maafa yanayotokana na mafuriko pindi mvua zinaponyesha kwa kuhakikisha wananchi wanawekwa katika mazingira salama.
Kunenge, alisema kuwa wananchi hao wamepewa viwanja bure bila kulipia gharama yoyote na kwamba kila mmoja anapaswa kufanya maandalizi mapema ya kuanzisha makazi katika eneo hilo ambalo litakuwa limeondoa kero ya mafuriko yaliyokuwa yakitokea muda mrefu.
” Leo tumefika hapa kwa ajili ya kufanya maandalizi ya tahadhali juu ya mvua za Elmino ambazo zimekuwa zikileta maafa kwa wananchi wetu na ukizingatia Mkoa wa Pwani umezungukwa na Bahari ya Hindi ambayo imekuwa ikijaa maji wakati wa mvua na hivyo kuleta athari kwa wananch”, alisema Kunenge
Kunenge, alieleza kata ya Muhoro imegawanyika sehemu mbili ambayo ni Mohoro Mashirika na Mohoro Kaskazini na kuna kituo cha afya ambacho mwaka 2021/2022 kilikabiliwa na changamoto ya mafuriko lakini tayari Serikali imelifanyiakazi jambo hilo.
Alisema,eneo walilopata limetolewa na Wakala wa Usimamizi wa Misitu na Mazingira (TFS) ambapo ndani yake kunajengwa huduma zote za jamii ikiwemo kituo cha afya,Shule,Soko , makazi na mahitahi mengine.
Kunenge alieleza,hupatikanaji wa viwanja hivyo imetokana na juhudi za Rais Dkt .Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye aliyeridhia kugawa eneo hilo kwa wananchi wake na kwamba hakuna budi ya kumshukuru kwa hatua hiyo kubwa.
“Niwaombe wananchi wa Mohoro muungeni mkono Rais Samia kwa hatua hii kubwa aliyoifanya kwa kuhakikisha wote tunahamia katika maeneo tuliyopangiwa na sisi leo tumekuja kuwahamasisha ili muweze kuhama mapema,” anasema Kunenge
Katika hatua nyingine Kunenge , alifafanua mbali na hatua ya kugawa viwanja bure lakini pia tayari Serikali ipo katika mpango wa kujenga daraja jipya la Mohoro ambalo mara nyingi wakati wa mvua hujaa maji na hivyo kuleta maafa.
Alisema ujenzi daraja hilo tayari usanifu umefanyika na sasa imefikia hatua ya manunuzi na kwamba mkandarasi akipatikana Novemba mwaka huu daraja litaanza kujengwa.
Hata hivyo ,wananchi waliipongeza Serikali kwa uamuzi wao na kukubali kuhama.
Walieleza,hatua hii ni njema kuchukua ,kufanya maandalizi juu ya kuwasaidia wananchi kuepukana na maafa yanayotokana na mvua za Elnino kama ambavyo imetangazwa na mamlaka za Hali ya Hewa Nchini( TMA).
Mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Mohoro Said Hamisi , aliishukuru Serikali kwa hatua kubwa ya kuwahamisha katika eneo hilo na kuwapa viwanja bure ambapo amesema wataitumia nafasi hiyo vizuri kwa ajili kujenga makazi yao ya kuishi.
Hamisi,alisema katika jambo kubwa ambalo Serikali imefanikiwa ni kuwatengenezea wananchi mazingira mazuri ya kuishi kwani walikuwa wanapata shida kubwa ya kupoteza ndugu zao, watoto na kupoteza mali zao wakati mafuriko yakitokea.