Na Issa Mwadangala.
Wanafunzi wa shule ya sekondari ya Bweni God’s Bridge Songwe wamemuuliza Kamanda wa Polisi mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Theopista Mallya watawezaje kutoa taarifa za ukatili wanazofanyiwa na wazazi au walezi wao ikiwa wanawategemea katika malezi yao kwa kuwasomesha na kuwapatia mahitaji yao ya msingi.
Akijibu maswali ya wanafunzi hao Oktoba 19, 2023 aliwaambia kuwa kuna Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia Wanawake na Makundi Maalum ipo kwa ajili ya kuwasaidia watoto waliopata matatizo kama hayo “nawasihi msiogope wala kusita kutoa taarifa za ukatili mnazofanyiwa, taarifa hizo zitasaidia kuwachukulia hatua wazazi wanaofanya vitendo hivyo ikiwemo kufikishwa mahakamani”
Hata hivyo, Kamanda Mallya alitoa elimu ya kuwajenga wanafunzi hao kwa kuzitambua haki zao,nini maana ya ukatili,madhara yake ikiwa ni pamoja na namna ya kutoa taarifa sehemu mbalimbali kama Polisi,kwa Walimu wao, kwa Viongozi wa dini na kwa Wenyeviti wa maeneo yao vilevile aliwaambia zipo sheria mbalimbali zinazolinda haki za watoto kwa kuzingatia usawa wa kijinsia sambamba na haki za msingi kwa mtoto.
Wanafunzi mbalimbali mkoani Songwe wameendela kunufaika kutokana na jitihada kubwa zinazofanywa na Jeshi la Polisi mkoani humo kutembelea mashuleni na kuwajenga wanafunzi kuhusu umuhimu wa Jeshi la Polisi na kazi wanazofanya na namna linavyopambana na vitendo vya kihalifu kwenye jamii.