Na. Mwandishi wetu-Dar es salaam
Wanafunzi wa chuo cha Taifa cha Utalii nchini Tanzania (NCT) wanatarajiwa kuanza kufanya mazoezi ya utendaji kazi katika nchi za Denmark, Norway, Ujerumani na Sweden.
Haya yamebainishwa na Mkuu wa Chuo hicho, Dkt. Florian Mtey baada ya kutembelewa na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Bixter.work, Bi. Nataliya Jorgensen na Mkuu wa Kituo cha SUGECO Bw. Revocatus Kimario ofisini kwake jijini Dar es salaam.
Dkt. Mtey amebainisha kwamba fursa hii ambayo wanafunzi wa chuo hicho cha Utalii wanaenda kuipata italeta tija katika fani ya ukarimu kwa vile kwa sasa soko la utalii nchini limekuwa kubwa kutokana na juhudi kubwa zilizofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia filamu ya kutangaza utalii ya The Tanzania Royal Tour.
Awali, wakitembelea chuo hicho katika Kampasi ya Dar es Salaam, Bi. Nataliya kutoka Bixter.work na Bw. Kimario kutoka SUGECO kwa pamoja wamefurahi sana kuona Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) kinatumia vifaa bora na vya kisasa kutoa mafunzo ya Ukarimu na upishi, na kwamba kwao itakuwa ni fursa kubwa kwa kuchangia mafunzo ya wataalamu wa ukarimu katika nchi ya Tanzania