Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu za Kilimo nchini ASA, Dkt. Sophia Kashenge, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uwekezaji wa kiasi kikubwa cha fedha kwa wakala, jambo ambalo limeongeza uzalishaji wa mbegu na kuwawezesha wananchi kupata mbegu bora kwa bei nafuu.
Uwekezaji huu katika uzalishaji wa mbegu bora umeleta mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo nchini. Miaka mitano iliyopita, uzalishaji wa mbegu kupitia ASA ulikuwa tani 500, lakini sasa umefikia tani 3500. Idadi ya mashamba ya wakala imeongezeka kutoka mashamba 8 hadi 16. Awali, asilimia 12 tu ya mashamba haya yalikuwa yakilimwa, lakini sasa ni karibu asilimia 90. Aidha, kufuatia uwekezaji uliofanywa katika shamba la mbegu eneo la Kilimi katika wilaya ya Nzega kuanzia mwaka ujao shamba hilo litaweza kuzalisha mbegu mara mbili kwa mwaka na hivyo kuongeza unafuu zaidi kwa wakulima.