Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Afrika na Mawaziri wa nchi za Nordic wakubaliana kuimarisha biashara na uwekezaji, kubadilishana ujuzi, teknolojia pamoja na kukuza uwekezaji baina ya nchi hizo.
Makubalianao hayo yameafikiwa wakati wa Mkutano wa 20 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Nordic unaoendelea Jijini Algiers, Algeria ambapo mkutano huo ulianza tarehe 16 – 18 Oktoba 2023.
Akizungumza baada ya makubaliano hayo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Y. Makamba (Mb.) amesema kuwa mkutano huo umekuwa na mazungumzo ya tija kuhusu ushirikiano wa kuimarisha biashara na uwekezaji kati ya Afrika na nchi za Nordic, kubadilishana ujuzi, teknolojia pamoja na kukuza uwekezaji.
“Tumekuwa na mazungumzo yenye tija yanayolenga kuimarisha biashara na uwekezaji kati ya nchi Afrika na nchi za Nordic, kubadilishana ujuzi, na teknolojia pamoja na kukuza uwekezaji baina ya nchi zetu,” alisema Mhe. Makamba.
Waziri Makamba ameongeza kuwa katika mkutano huo, Mawaziri wa nchi za Afrika na Nordic wamekubaliana kufanya kazi kwa bidii ili kuchochea ongezeko la uwekezaji kati ya nchi hizo.
“Nimepata bahati ya kuwa Mwenyekiti katika mjadala wa uliohusu ushirikiano wa biashara na uwekezaji kati ya nchi za Afrika na Nordic na tumekubaliana kuna kazi kubwa ya kufanya kuongeza uwekezaji na biashara kati ya nchi zetu na kuna maazimio yatatoka kuhusu masuala hayo ambayo ndiyo yatatuongoza kuanzia sasa kuhusu nini tunafanya ili nchi yetu ya Tanzania na nchi zetu za Afrika zipate mitaji zaidi, ujuzi zaidi, teknolojia zaidi, na ifanye zaidi biashara na nchi za Nordic,” aliongeza Waziri Makamba.
Awali akifungua Mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria, Mhe. Ahmed Attaf alisema kuwa Afrika inaendelea kujizatiti kuimarisha zaidi ushirikiano wake na nchi za Nordic kwa maslahi mapana ya pande zote hususan katika vipaumbele kwenye masuala ya amani na usalama, biashara na uwekezaji, na elimu ya ufundi ili kuwawezesha vijana kupata ujuzi na maarifa.
Akiongea kwa niaba ya Nchi za Nordic, Waziri wa Mambo ya Nje wa Denmark, Mhe. Lars Løkke Rasmussen alisema kuwa Nordic itaendelea kushirikiana na Umoja wa Afrika (AU) na Afrika kwa ujumla katika kuhakikisha kuwa amani na usalama vinaendelea kudumishwa.
Mhe. Rasmussen aliongeza kuwa Nordic itaendelea kuhakikisha kuwa ulinzi na usalama Barani Afrika vinapewa kipaumbele, ufadhili endelevu wa mfuko wa amani na usalama wa Umoja wa Afrika; kuboresha sera zinazohusu maendeleo ya vijana ili waweze kuchangia kwenye maendeleo ya jamii.
Pamoja na mambo mengine, mkutano huo umejadilia masuala ya ulinzi na usalama hususan kwenye mapambano dhidi ya ugaidi na mageuzi katika Umoja wa Mataifa; kuweka mikakati ya kuboresha elimu Barani Afrika; kukuza biashara na uwekezaji baina ya pande mbili na umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kimataifa ili kukabiliana na changamoto zinazoikabili dunia kwa sasa ambazo zinahitaji ushirikiano ili kuzitatua.
Mkutano kati ya nchi za Afrika na Nordic ulianza mwaka 2000 ambapo mwaka 2001 Mkutano wa kwanza ulifanyika nchini Sweden na imekuwa ikifanyika kwa kupokezana kati ya nchi za Nordic na Bara la Afrika.
Imwaka 2019, Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa 18 kati ya Nordic na Afrika mwaka 2019 ambapo nchi 34 zilishiriki katika mkutano huo. Tanzania ni moja kati ya marafiki wakubwa wa nchi za Nordic na imekuwa ikishiriki mikutano ya Afrika – Nordic inapokuwa ikifanyika. Mkutano wa mwaka 2022 kati ya Nchi za Afrika na Nordic ulifanyika mwezi Juni 2022 Helsinki, Finland.