Mkurugenzi metendaji wa FCS Francis Kiwanga, akizungumza katika Mkutano na Waandishi wa Habari kuelekea Wiki ya Asasi za Kiraia inayotarajiwa kuanza rasmi Oktoba 23 hadi 27, 2023 Jijini Arusha
………………….
Na Mwandishi wetu
Washiriki wapatao 500 wakiwemo wadau wakuu wa maendeleo wa Asasi za kiraia pamoja na Sekta Binafsi, wanatarajiwa kushiriki katika wiki ya Asasi za Kiraia (AZAKI), itakayofanyika kuanzia Oktoba 23 hadi 27, 2023 Jijini Arusha.
Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation For Civil Society (FCS), Francis Kiwanga, ameyasema hayo leo Oktoba 17, 2023 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam.
Amesema kuwa wiki hiyo inaendeleza juhudi zake katika kuhakikisha ushirikishwaji bora na watendaji kutoka sekta mbalimbali hapa nchini.
“Tukio hili ni muhimu kwa wadau wa maendeleo ya watu na Taifa kwa ujumla, katika kuimarisha mahusiano na ushirikiano baina ya wadau mbalimbali wa maendeleo ikiwemo Sekta Binafsi, Serikali na wananchi.
“Tukio hili Kwa mwaka huu limejikita katika kujadili na kuweka mikakati na kuboresha utendaji wa AZAKI nchini haswa katika masuala ya Teknolojia” amesema Kiwanga.
Aidha Kiwanga ameeleza kuwa katika wiki hiyo mijadala mbalimbali itajadiliwa, ikiwemo ya kuziwezesha na kuzipa nguvu jamii zilizotengwa, ujumuishwaji wa teknolojia kwenye kazi za AZAKI, utetezi, ushirikiano na uchechemuzi wa kidigitali, Data takwimu kwaajili ya kuleta mabadiliko, Teknolojia, maadili, pamoja na ubunifu wa Teknolojia na maendeleo endelevu.
Akifafanua zaidi, Kiwanga amesema, katika wiki hiyo kutakuwa na mada tofauti zilizojikita katika kutathimini kaulimbiu ya Teknolojia na AZAKI ambazo ni pamoja na ujumuishaji na uwekezaji wa kidigitali, matumizi ya takwimu kuleta manufaa kwa jamii, teknolojia na utetezi wa kijamii, elimu na mafunzo ya dijitali nchini Tanzania .
Nyingine ni pamoja na teknolojia katika ushirikiano na kuboresha uwazi, ujasiriamali na teknolojia kwa maendeleo endelevu, kuimarisha usalama mtandaoni, kuwawezesha wanawake na vijana kupitia teknolojia, kuweka wazi data na uwazi kwenye Utawala, pamoja na kutumia maarifa bandia yanayozingatia maadili Kwa manufaa ya jamii.
Kwa upande wake mshauri mwandamizi kutoka Shirika Norwegian Church, Aneth Torjusen amesema kikao hicho pia kinalenga kujadili athari za mikopo inayotolewa na Serikali katika maisha ya watu na maeneo yanayopendekezwa kuboresha.
Naye Mkuu wa kitengo cha sekta za umma kutoka Benki ya Stanbic Doreen Dominic amesema sekta binafsi inalojukumi kubwa la kuwanyanyua wananchi katika shughuli za kiuchumi Kwa kuwawezesha katika kazi zao za ujasiriamali ikiwemo biashara.
Wiki ya AZAKI inaendeleza juhudi zake katika kuhakikisha ushirikishwaji bora na watendaji kutoka sekta mbalimbali hapa nchini.