Meneja Idara Shughuli za Takwimu Taifa Benedict Mugambi.
Vijana wakiendelea kupewa Semina ya usambazaji na matumizi ya matokeo ya Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.
Kaimu katibu tawala msaidizi Mkoa wa Mwanza Chagu Nghoma akizungumza wakati wa kufungua mafunzo ya siku moja kwa vijana ya usambazaji na matumizi ya matokeo ya Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022
…………
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Chagu Nghoma amewataka vijana kutumia Takwimu za matokeo ya Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kujikita kwenye Sekta zenye tija ili kujiimarisha na kujiinua kiuchumi.
Ametoa rai hiyo Jana wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku moja kwa vijana juu ya usambazaji na matumizi ya matokeo ya Sensa ya watu na makazi yaliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
Amesema vijana ndio kundi linalotegemewa kuchagiza uchumi wa nchi kwa sasa na siku zijazo hivyo ni wanatakiwa kuwa na taarifa sahihi za maeneo yenye tija ambapo kutakuwa na biashara,kilimo au uvuvi na kwamba majibu ya suala hilo yanapatikana kwenye Takwimu zilizokusanywa wakati wa Sensa.
“Suala la ajira kwa vijana ni changamoto hivyo tunamshukuru sana Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kuwapa mafunzo kundi hili kwani wataweza kutumia Takwimu hizo kuona sehemu gani ina fursa ya kujiinua kiuchumi”, amesema Nghoma.
Aidha, ametumia wasaa huo kumshukuru Rais Samia kwa kuweka fedha nyingi kwenye miradi ya kuwainua vijana kiuchumi ikiwemo ujenzi wa kesho bora kwenye kilimo na Mifugo (BBT).
Kwa upande wake Mtakwimu mwandamizi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Mdoka Omary, amesema kuwa mafunzo hayo ni katika utekelezaji wa muongozi uliozinduluwa na Rais Samia wa kuhakikisha matokeo hayo yanasambazwa katika ngazi zote ili takwimu hizo ziwafikie wananchi wote.
Ameeleza kuwa matokeo ya Sensa ya watu na Makazi yanatoa majibu na fursa ya eneo gani liongezewe nguvu katika kuleta maendeleo ya haraka kwenye jamii.
Nao baadhi ya vijana walioshiriki mafunzo hayo wamesema yatawasaidia kwenye kutafuta fursa mbalimbali ili waweze kujiinua kiuchumi.