MPANGO wa Kampuni ya Scancem International DA kununua Kampuni ya saruji ya Tanga kwa mara nyingine umegonga mwamba kufuatia hukumu ya karibuni ya Baraza la Ushindani (FCT) kutengua uamuzi wa Tume ya Ushindani (FCC) uliobariki uunganishwaji wa kampuni hizo.
Licha ya FCC na serikali kuonekana kubariki mpango wa Scancem kununua hisa za Tanga Cement, kampuni hiyo ya Ujerumani itabidi kusubiri zaidi kuona iwapo itafanikiwa kutimiza ndoto yake kutokana na matakwa ya kisheria.
Mnamo February 28, mwaka huu, FCC ilikubali maombi mapya yaliyowasilishwa na Scancem International DA ya kununua hisa asilimia 68.33 za kampuni ya Tanga Cement, baada ya maombi ya awali kuzuiwa na FCT kufuatiwa rufani iliyowasilishwa na wadau wa saruji na Chama cha Kuteteta Walaji Tanzania.
Uamuzi huo ulipingwa na mmoja wa wadau wa Saruji Peter Hellar, aliyekata rufaa Baraza la Ushindani akidai FCC ilifanya kosa la kuidharau mahakama kwa kuridhia maombi mapya ya Scancem International DA licha ya kuwepo kwa zuio la kwa mchakato wa uuzwaji wa Tanga Cement lililotokana na hukumu iliyotolewa na FCT mnamo Septemba 23, 2022 dhidi ya uamuzi wa FCC wa kukubali maombi ya awali ya Scancem International DA kutaka kununua hisa asilimia 68.38 za Tanga Cement ya mwezi Aprili, 2022.
Katika uamuzi wake wa Oktoba 16, 2023, FCT chini ya uenyekiti wa Jaji Fatma Maghimbi, iliamua kwamba madhali FCT ipo kwa ajili ya kusimamia na kurekebisha mwenendo na uamuzi wa FCC, haikuwa sahihi kuwapo maamuzi mawili yanayopingana kutoka kwenye vyombo hivyo katika suala moja, ikizingatiwa FCT ilipata awali kuzuia muungano wa kampuni hizo.
Alisema FCT baada ya kupitia hoja za pande zote zinazohusika imefutilia mbali uamuzi wa FCC wa kuridhia maombi mapya ya Scancem International DA ambayo yalikuwa yakikinzana na uamuzi wa FCT uliozuia mchakato wa uuzaji Tanga Cement kwani ulikuwa unakiuka sharia za ushindani, zinazozuia kampuni moja kumiliki zaidi ya asilimia 35 ya hisa katika soko.
Jaji Maghimbi alisisitiza umuhimu wa kuvutia na kulinda wawekezaji na kuheshimu utawala wa sharia na ushindani wa kibiashara, Jaji Maghimbi, ambaye ni Mwenyekiti wa FCT, aliwataka Scancem International, iwapo wanahitaji kuendelea na mchakato wa kununua hisa za Tanga Cement, kuiomba FCT kurejea uamuzi wake wa awali wa September 23, 2022, na maombi hayo yafanyike ndani ya siku 21 tangu kutolewa kwa hukumu ya sasa.
Uamuzi huu ni pigo jingine kwa Kampuni ya Scancem, kampuni tanzu ya Heidelberg Cement AG, inayomiliki Twiga Cement, ambayo imekuwa ikifanya juhudi kununua asilimia 68.33 za AfriSam Mauritius Investment Holdings Limited, inayomiliki Tanga Cement tangu mwaka 2021.