Mbunge wa Tanga Mjini Mhe. Ummy Mwalimu tarehe 15/10/2023 ameshiriki mkutano wa hadhara kata ya Msambweni.
Katika mkutano huo, Mhe Ummy aliwaelezea wakazi wa Msambweni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ambapo alitoa Taarifa Miradi mbalimbali iliyotekelezwa na Diwani wa kata hiyo Mhe Godius Kimathi na Mbunge chini ya Uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan. Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya Elimu katika Shule za Msingi na Sekondari Msambweni, ujenzi wa barabara za kiwango cha lami na changarawe katika mitaa ya Msambweni sambamba na uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Aidha Mhe Ummy alielezea jitihada zilizofanyika katika kuimarisha huduma za umeme, maji na masoko katika Jiji la Tanga. Hata hivyo Mhe Ummy alieleza kuwa maendeleo ni mchakato hivyo yeye na Diwani Kimathi wataendelea kutatua kero za wananchi wa Msambweni ikiwemo kutatua ukosefu wa Zahanati katika Kata hiyo.
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali akiwemo Ndugu Hamza Bwanga, Mwenyekiti wa Jumuia ya wazazi wilaya ya Tanga, Wajumbe wa Kamati ya Siasa Wilaya, Kaimu Katibu wa CCM Wilaya Ndugu Urasa Nanyaro, Waheshimiwa Madiwani, wajumbe wa kamati ya siasa Kata ya Msambweni wakiongozwa wa Katibu wa CCM Kata ya Msambweni Ndugu Joyce Kimweli viongozi na wananchi wa Tanga.