Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma ameiagiza Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) ihakikishe kuwa inaandaa mpango kazi wa utekelezaji wa majukumu kutoka Kampuni ya kukusanya mirabaha ya kazi za muziki iliyopewa Leseni ijulikanayo kama Tanzania Music Rights Society (TAMRISO).
Aidha, ameitaka COSOTA ihakikishe kuwa inaifuatilia Kampuni hiyo ili iwasilishe mfumo wa ufuatiliaji wa matumizi ya kazi za Muziki katika maeneo mbalimbali kabla ya mwisho wa mwezi Oktoba 2023.
Mhe. Mwinjuma ametoa maagizo hayo leo Oktoba 17, 2023 jijini Dar es Salaam wakati wa kikao chake na Afisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki Bi. Doreen Anthony Sinare alipotembelea Ofisi hiyo kupata mrejesho wa utendaji wa TAMRISO.
” Suala la TAMRISO kuwa na mfumo ni muhimu sana kwa sababu mfumo ndiyo unaosaidia kujua nani amepata kiasi gani kulingana na matumizi ya kazi yake na Wasanii wengi wemekuwa wanalalamikia hili hivyo ni lazima walete taarifa ya mfumo huo,” amesisitiza Naibu Waziri Mhe. Mwinjuma.
Naibu Waziri Mwinjuma ameipongeza COSOTA kwa kukamilisha mchakato wa kuwezesha makusanyo ya Tozo ya Hakimiliki ( Blanktape Levy) kuanza kufanyika akieleza kuwa Wizara itaendelea na mchakato wa kuliomba Bunge riridhie baadhi ya vifaa ambavyo havijaingizwa kwenye orodha ya awali vyenye matumizi makubwa katika kazi za sanaa ikiwemo Kompyuta, Simu, Flash, Harddrive, Vishikwambi na vinginevyo lengo likiwa ni wasanii kunufaika na tozo hii kiuchumi.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki nchini Doreen Sinare ameeleza kuwa Ofisi yake itaendelea kusimamia haki za Wasanii pamoja na ukusanyaji wa mapato.
“Tumetoa tangazo la kuongeza siku za wadau kuomba Leseni ya Kampuni ya kukusanya mirabaha kwa madaraja ambayo yalikuwa bado hayajaomba kama wadau wa Filamu, Sanaa za Ufundi, Wachapishaji wa Vitabu na Sanaa za Maonesho na mwisho wa kuwasilisha maombi hayo ni tarehe 02 Novemba, 2023.”
.