Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Y. Makamba (Mb.), amewasili nchini Algeria kushiriki Mkutano wa 20 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Nordic utakaofanyika tarehe 16 – 18 Oktoba 2023, Jijini Algiers, Algeria.
Mara baada ya kuwasili nchini Algeria, Mhe. Makamba alipokelewa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Houari Boumediene Jijini Algiers na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Diaspora ya Algeria, Bw. Lounes Magramane.
Mkutano wa 20 wa nchi za Afrika na Nordic unahusisha nchi tano (5) za Nordic ambazo ni Finland, Sweden, Denmark, Norway na Iceland pamoja na nchi 25 za Afrika ambazo ni marafiki (wenye ushirikiano na Nordic) wa Nordic.
Mkutano kati ya nchi za Afrika na Nordic ulianza mwaka 2000 ambapo mwaka 2001 Mkutano wa kwanza ulifanyika nchini Sweden na imekuwa ikifanyika kwa kupokezana kati ya nchi za Nordic na Bara la Afrika.
Itakumbukwa kuwa Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa 18 kati ya Nordic na Afrika mwaka 2019 ambapo nchi 34 zilishiriki katika mkutano huo.
Tanzania ni moja kati ya marafiki wakubwa wa nchi za Nordic na imekuwa ikishiriki mikutano ya Afrika – Nordic inapokuwa ikifanyika. Mkutano wa mwaka 2022 kati ya Nchi za Afrika na Nordic ulifanyika mwezi Juni 2022 Helsink, nchini Finland.