Na Sophia Kingimali
WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) imepanga kuzishirikisha sekta binafsi katika miradi yake ili kusaidia kuondoa changamoto ya nyumba kwa watumishi wa umma na wananchi kwa ujumla
Akizungumza jijini Dar es Salaam Oktoba 16, baada ya kutembelea miradi mitatu ya TBA, Mkurugenzi wa Idara ya Miliki TBA, Said Mndeme amesema kuwa mahitaji ya nyumba yamekuwa yakiongezeka kila mwaka kwa zaidi ya 300,000 kutokana 200, 000 hivyo wamejipanga kushirikisha sekta binafsi wameanza kuandaa orodha ya miradi kwa nchi nzima ili waweze kushirikiana na sekta binafsi.
“Machi mwaka jana Rais Dk.Samia Suluhu Hassan wakati wa uzinduzi wa nyumba za Magomeni Kota, alitutaka TBA na taasisi nyingine za Serikali zinazioshughulikia ujenzi wa makazi ya watu kushirikiana na sekta binafsi za nje au ndani kwani Kwa kufanya hivyo zitaweza kuendeleza makazi bora kwa haraka kuliko kusubiri Serikali kukusanya fedha ambazo haziwezi kukidhi uhitaji wa haraka wa makazi hayo, ” amesema.
Amesema agizo hilo la Rais Dk. Samia liliungwa mkono na wabunge ambao waliishauri TBA, kushirikiana na sekta binafsi ili kuongeza uwezo wa kujenga nyumba nyingi zitakazosaidia kupunguza uhaba kwa watumishi wa umma badala ya kuendelea kutegemea ruzuku ya serikali.
Ameongeza kuwa machi mwaka huu Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu iliishauri TBA kuanza kujiendesha kibiashara kwa kushirikiana na Sekta Binafsi na kuacha kutegemea fedha za ruzuku kutoka Serikalini kutekeleza miradi yake.
Mndeme amesema kwa miaka iliyopita mahitaji ya nyumba yalikuwa yakiongezeka taratibu ila kwa sasa uhitaji ni mkubwa.
“Kwa sasa tunakamilisha miradi hii taratibu kwa kuwa Serikali imepitisha mabadiliko ya kuturuhusu kushirikiana na sekta binafsi, tutatoa orodha ya miradi yote Tanzania nzima na tutawakaribisha sekta binafsi ili kuweza kuja kushirikiana na sisi katika uendelezaji wake,”amesema.
Amesema yapo maeneo mengi ambayo hivi karibuni watayatangaza na kuzikaribisha sekta binafsi kushiriki katika kuyaendeleza.
“Eneo la Canadian village tunatarajia kujenga majengo 23 yatakayobeba familia 472 na nyumba hizi zitatumiwa na wananchi wote, hivyo tunazikaribisha sekta binafsi kushirikiana kuendeleza eneo hilo,” amesema .
Pia ameongeza kuwa kabla ya mwaka huu kuisha wanatarajia kutangaza miradi mipya katika eneo hilo la Canadian lililopo Masaki, Dar es Salaam.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja TBA Mkoa wa Dar es Salaam, Benard Mayemba amesema utekelezaji wa miradi ya Dar es Salaam inakwemda vizuri hivyo nimatumaini yao miradi itakapokamilika itatatua changamoto ya nyumba za makazi kwa watumishi wa umma na wananachi wote kwa ujumla.
” huu ujenzi wa nyumba awamu ya pili zilizopo magomeni Kota utekelezaji wake ni asilimia 83 na nyumba hizo zitakaliwa na wananchi wa kipato cha kati kuelekea juu ,” amesema.
TBA inaishukuru serikali kwa kutoa kiasi cha sh.bilioni 69.2 Kwa ajili ya miradi ya maendeleo pekee ikiwa pamoja na ukarabati wa majengo.kutokana na uwepo wa ongezeko hilo,mahitaji ya nyumba yamekuwa makubwa, hivyo wanaangalia maeneo ya kuzishirikisha sekta binafsi katika kuendeleza miradi yao