Waziri wa Maendeleo ya Jamii ,Jinsia ,Wazee na Watoto Mhe. Riziki Pembe Juma akikata utepe kuashiria uzinduzi wa CD ya Tungo njema wakati wa hafla ya siku ya Tungo njema iliyoandaliwa na uongozi wa Redi Al-nour na kufanyika katika Ukumbi wa Skuli ya Sekondari Dkt.Ali Mohamed Shein Wilaya ya Mjini Unguja.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii ,Jinsia , Wazee na Watoto Mhe. Riziki Pembe Juma akizunguma na Wadau wa Sanaa za Mashairi kuhusiana na umuhimu wa kuelimisha jamii kupitia sanaa hiyo huko Ukumbi wa Skuli ya Sekondari Dkt.Ali Mohamed Shein Mjini Unguja.
Na Fauzia Mussa, Maelezo
Waziri wa Maendeleo ya Jamii ,Jinsia , Wazee, na Watoto, Mhe Riziki Pembe Juma amewataka wasanii wa tungo za mashairi kujikita katika kutunga tungo zenye kukemea maovu yaliomo katika jamii.
Akizungumza na watunzi,waghani na wapenzi wa mashairi katika hafla ya siku ya tungo njema iliyofanyika Skuli ya Sekondari Dkt.Ali Mohamed Shein amesema kufanya hivyo kutapunguza vitendo viovu kwani jamii ya walio wengi hufuatilia sanaa za mashairi ikiwemo tenzi na mashairi.
Alisisitiza kuwa kila mmoja ana jukumu la kukemea mambo maovu kwa namna moja au nyengine hivyo aliwataka wasanii kupitia tungo zao kujikita katika kuzungumiza maadili ya mzanzibar na kurekebisha pale ambapo maadili hayo yanapoporomoka.
Alisema ujumbe unaotolewa kupitia tungo hizo huifikia jamii kwa haraka zaidi hivyo aliwataka wasanii wa sanaa hiyo kushirikiana na Serikali katika kupinga vitendo vya udhalilisha kwani vinaonekana kuendelea kushamiri siku hadi siku.
Mhe Riziki alifahamisha kuwa udhalilishaji sio kubakwa tu hata kutamkiwa maneno yasiofaa ni udhalilishaji,hivyo aliwataka watunzi wa tungo njema kutumia elimu, ubunifu na ujuzi wao katika kukemea vitendo hivyo visitokee hasa kwa wanawake,mayatima na wenye mahitaji maalum.
Hata hivyo aliupongeza uongozi wa Redio Al-nour kwa kuandaa siku hiyo muhimu iliyowashirikisha watu tofauti ikiwemo mayatima na wenye mahitaji maalum.
Awali Mhe. Riziki alichukua fursa hiyo kuitaka jamii kuuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Huseein Ali Mwinyi katika kuwaletea maendeleo wananchi wake nakuwataka kuendelea kudumisha amani na utulivu kwa ajili ya maendeleo zaidi.
Mkurugenzi Baraza la KiswahiIi Zanzibar Dkt.Mwanahija Ali Juma amesema BAKIZA itaendelea kuunga mkono juhudi za wasanii wa mashairi kwani wamekuwa na mchango mkubwa katika kuiendeleza na kuikuza lugha hiyo.
Amesema wasanii hao ni kundi ambalo halipaswi kuachwa nyuma kwani wamekuwa na mchango mkubwa katika kuchangia kuelimisha na kuikosoa jamii juu ya mambo mbalimbali yanayotokezea Nchini.
“Mashairi hayo hutolewa kwa Kiswahili na hupokelewa na hadhira mbalimbali ndani na nje ya Nchi hiyo ni njia moja ya kukisambaza kiswahili,hivyo ipo haja kukuza na kuendeleza vipaji vyao ili sanaa hiyo iendelee kutumika siku hadi siku”alifahamisha Dkt.Mwanahija
Akisoma Risala ya washairi Omar Khamis amesema Dhamira kuu ya tungo njema ni kukemea ,kushajihisha,kukosoa na kuelemisha juu ya mambo mbalimbali yanayotokea katika jamii.
Aidha alisema kupitia tungo za mashairi wamefanikiwa kuchochea maendeleo katika jami kwa kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari , kupinga vitendo vya udhalilishaji, kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kutunza amani pamoja na kujenga mahusiano mazuri ya Taasisi za Serikali na Binafsi.
Awali alifahamisha kuwa madhumuni ya siku ya tungo njema ni kutambua na kuthamini juhudi na mchango wa wasanii wa mashairi na tenzi katika kujenga jamii iliyobora
Maadhimisho hayo ni ya pili kufanyika ambapo kwa mwaka yameshirikisha wadau mbali mbali wa Tungo njema,Watoto yatima na watu wenye mahitaji maalum.