Maelefu kutoka ndani na nje ya nchi wameguswa na historia ya Sister Gracia Mligo aliyeishinda vita ya shinikizo la ndoa ya utotoni pamoja na imani za kishirikina katika kijiji cha Kisilo wilayani Njombe kwa kuanza kuipigania ndoto ya Utawa na kisha kuja kufanya mageuzi ya uzazi mpango kwa wananchi waliyositisha mpango wa kuzaa kwa muda.
Katika ibada ya jubileo ya Miaka 25 ya sista hiyo viongozi akiwemo Padre Fredrick Mwabena wanasema Kabla ya Miaka ya 90’S Kijiji cha Kisilo hakikuwa na kiongozi wa kiimani kwasababu kilitawaliwa na imani za kishirikina na mila kandamizi kwa mtoto wa kike lakini kitendo cha Mtawa huyo kufikia hatima yake kimefungua milango kwa watu wengine ambapo hadi sasa kuna Masista na Mapadre kijijini kwao.
Fr Mwabena amesema miaka ya Nyuma katika kijiji chao wazazi walikuwa wanaozesha mtoto wa kike punde baada ya kuhitimu darasa la saba vita ambayo aliishinda Mtawa huyo na kisha kuvunja mwiko wa miaka mingi.
Awali akieleza mchango wa Mjubilanti Sista Gracia Mligo katika maendeleo ya Kijiji cha Kisilo na Kigango chao Katekista Valerian Mwalongo amesema kuna wakati serikali ilikuja kutoa elimu ya uzazi wa mpango kijijini kwao na kupokelewa kwa asilimia 100 na wananchi hatua ambayo ikapelekea kukosekana kwa watoto mashuleni na nguvu kazi mtaani ,hali ambayo ikamlazimu Sista Mligo kuja tena kutoa elimu hiyo.
“Tunashukuru akina mama wameanza kuzaa tena baada ya sista Gracia kuja kuelimisha kijiji chetu juu ya matumizi ya uzazi wa mpango kwa njia za asili ,kwasababu Serikali iilipokuja kutufundisha uzazi wa mpango watu walielewa vizuri na wakawa hawazai hadi shule zikakosa wanafunzi ,alisema Katekista Valerian Mwalongo”
Kwa pande wao wakazi wa kijiji cha Kisilo akiwemo Sholastica Mligo nje ya kanisa la Katoriki Kigango cha Kisilo wanasema Mtawa huyo anayetimiza miaka 25 ya utumishi wake kiroho amekuwa na faida kubwa kwa wakazi wa kisilo na kata ya Lugenge kwa ujumla wake kwasababu amewafundisha ushumi wa parachichi na kisha kuleta watalaamu ambao aliungana nao kutoa elimu ya matumizi bora ya uzazi wa mpango.
Wamesema kabla ya mjubilanti huyo kuja kuwaelimisha walikuwa wamepatiwa elimu na maofisa wa serikali juu ya uzazi wa mpango na kuelewa kwa kina hatua ambayo ilipelekea familia nyingi kusitisha uzazi na kupunguza idadi ya watoto mtaani na mashuleni.
“Kwakweli mtumishi huyu amefanya mageuzi kwetu kwasababu tuliacha kuzaa hadi shule zikakosa wanafunzi,Unakuta darasa lina watoto saba lakini tangu amekuja kuelekeza uzazi wa mpango wa asili magonjwa ya uvimbe yamepungua na wameanza kupata watoto ili wakazijaze shule,alisema Sholastica Mligo mkazi wa Kisilo”
Aidha wamesema amewafundisha masuala ya afya ,elimu na uchumi wa parachichi hatua ambayo imewaongezea misuli ya uchumi wa familia.
Kwa upande wake Sista Gracia Mligo ambaye anaadhimisha jubilei ya miaka 25 ya Utawa amewashukuru watu wote waliyojumuika katika sherehe hizo na kisha kutoa siri ya kufikia ndoto yake ya kuwa Mtawa ni malezi yenye maadili kutoka kwa wazazi wake pamoja na mchango mkubwa wa walezi wa kiroho kumpa miongozo ya dini.
Amesema kabla ya kuweka wazi mpango wake wakusomea Utawa alikuwa akipendezwa na kuvutiwa na mwonekano wa Mapadre wakiwemo wajomba zake hivyo na yeye alitamani siku aje kuvaa kanzu la Utawa na kisha kuja kuiweka bayana shauku yake hiyo kwa mlezi wake wa kiroho Padre Chrispin Mligo aliyekuwa Mafinga Wilayani Mufindi.
Kuhusu miongozo ya Utawa Sista Gracia Mligo anawataka ndugu jamaa na marafiki kuto andamana pindi atakapofariki dunia kwani shirika la masista limeweka bayana miongozo yake kwamba yeyote atakaefariki dunia atazikwa katika nchi ambayo umauti utakuwa umemfika.
“Ukiona vyaelea ujue vimeundwa ‘hivyo nawashukuru watu wote mliochangia kwa namna moja ama nyingine katika kufikia ndoto yangu ya Utawa ambayo mwanzoni sikumweleza yeyote zaidi ya kutamani maisha na mavazi ya mapadre husuani Mjomba wangu,alisema Sista Gracia Mligo”