Kamanda wa Polisi mkoa wa Songwe ACP Theopista Mallya, amewataka waamini wa kanisa la T.A.G Bethlehem Revival Temple kuendelea kufanya matendo mema na kukemea matendo maovu wanapokuwa kanisani mpaka kwenye himaya zao ili kupunguza vitendo viovu katika jamii.
Kamanda Mallya ameyasema hayo Oktoba 14, 2023 wakati akitoa elimu ya Ushirikishwaji wa Jamii katika Mkutano wa Injili ulioandaliwa na kanisa hilo eneo la Mlowo wilaya ya Mbozi.
“Tumshike Mungu waamini wenzangu na kuyatenda yale yote aliyoyaelekeza katika biblia takatifu pia kuyaishi ili kutokomeza vitendo viovu katika jamii zetu na kwa umoja wetu tusijihusishe na vitendo vya uhalifu na ukatili ikiwa ni pamoja na unyanyasaji kwa watoto” Alisema Kamanda Mallya.
Kamanda Mallya aliendelea kuwasihi waamini wa kanisa hilo walioudhuria katika mkutano huo wa Injili kuacha ulevi uliopindukia na kutoamini imani gombanishi za kishirikina kwani kufanya hivyo kutapunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji katika mkoa wetu.
Kwa upande wa waamini wa kanisa hilo wamepongeza elimu iliyotolewa na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa dhati kwa Jeshi la Polisi.