Na . Zillipa Joseph, Katavi.
Shirika la Uwakala wa m
Meli Tanzania (TASAC) limejipanga kutoa huduma bora za udhibiti wa Usalama Majini kwa wasafirishaji wa binadamu na mizigo kupitia bandari ya Karema iliyopo wilayani Tanganyika mkoani Katavi.
Bandari hiyo mpya ilijengwa kwa gharama ya shilingi bilion 47.9 ambayo imekamilika kwa asilimia 100 mpaka sasa imeweza kuhudumia mizigo tani 1,500.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Mkurugenzi wa Huduma Za Biashara ya Meli Bwana Nelson Mlali ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, aliwataka wafanyabiashara kianza kujiandaa kutumia bandari hiyo vema mara itakapokuwa imeunganishwa kwa barabara ya rami na reli ambayo Serikali ya awamu ya sita imepanga kuijenga.
Alisema TASAC ipo kwa ajili ya kuwahudumia katika kukagua vyombo vya usafiri majini na kuvisajiri na kutoa leseni kwa kampuni zinazotoa huduma bandarini, hivyo wasisite pale wanapopata changamoto zozote kuwasiliana na TASAC.
Kuhusu hali ya usalama katika ukanda huo wa ziwa Tanganyika alisema hali ni shwari na hakuna taarifa za matukio ya ya ajali majini ama vyombo kupata hitilafu na kusababisha adha kwa wasafiri.
Waziri wa Uchukuzi Mhe.Profesa Makame Mbarawa alisema serikali inaendelea na juhudi za kuhakikisha bandari hiyo inatumika kama lengo lake lilivyokusudiwa kwa kuinganisha na miundo ya uchukuzi.
Profesa Mbarawa ametaja maboresho yanayofanyika kuwa ni pamoja na kuweka lami katika kipande cha barabara ya urefu wa kilometa 110 ili kuwezesha magari ya mizigo kupita kwa urahisi.
Kingine ni Serikali kutengeneza meli mbili za mizigo na kukarabati meli za abiria zitakazokuwa zinatoa huduma kutoka Kigoma kupitia bandari ya Karema, Kasanga hadi nchi jirani za Zambia, DRC Congo na Burundi.
Aliongeza kuwa serikali ina mpango wa kujenga reli kutoka Mpanda mjini hadi Karema.
“Utaona sasa mipango yote hii ikikamilika bandari ya Karema itaweza kufanya kazi vizuri sana” alisema Mhe.Prof. Mbarawa.
Aliongeza kuwa Tanzania ina soko kubwa sana la kubeba mizigo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa Karema walisema kufunguka kwa bandari hiyo kutawawezesha kujiinua kiuchumi.
Wapo wafanyabiashara hapa wanakoboa mchele na kusafirisha kwenda Kongo kwa kutumia mitumbwi.
Wakazi hao waliongeza kuwa endapo itapatikana meli kubwa ya mizigo watanzania watanufaika zaidi.
“Kuanzia ng’ombe hadi mbuzi zote zinapelekwa Kongo na majahazi makubwa, hadi unga wa sembe” alisema Michael Kipata diwani wa Karema.