KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, imetoa rai kwa Ofisi ya Rais-TAMISEMI kuhakikisha inasimamia kwa weledi fedha zilizoletwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa TACTIC ili uweze kukamilika kwa wakati na kuleta tija kwa wananchi.
Hayo yamesemwa jijini Arusha na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe Denis Londo wakati wa ziara ya kamati hiyo kukagua mradi wa Dampo (Muriet), uwanja wa michezo Ngarenaro, Barabara ya Oljoro-Muriet na Barabara ya Bypass Kisongo-Airport ambapo miradi hiyo inasimamiwa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI.
Mhe Londo amesema Jiji la Arusha ni miongoni mwa maeneo yaliyobahatika kupokea fedha za mradi huo na hivyo kusisitiza kuwa ni vema fedha hizo zikatumika kwa weledi ili kutimiza azma ya serikali ya kuwahudumia wananchi wake.
” Arusha imebahatika kupata mradi huu ni matumaini yetu kuwa fedha hizi ambazo Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan amezitafuta na kuzileta basi zisimamiwe kwa weledi ili ziweze kukamilisha miradi hii kwa wakati na kuleta tija kwa Taifa letu,” Amesema Mhe Londo.
Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Deogratius Ndejembi ameiahidi kamati hiyo kuwa watahakikisha miradi hiyo inasimamiwa kwa weledi na kukamilika katika muda uliopangwa lengo likiwa kutimiza azma ya serikali ya awamu ya sita ya kuwahudumia wananchi wake.