Na MWANDISHI WETU
MKUU wa Wilaya ya Kaliua Dk. Rashid ChuaChua amewataka wananchi wa Wilaya hiyo hususani vijana kutafuta mbadala wa tatizo la nguvu za kiume ikiwemo kuzingatia vyakula vya lishe na kuacha kisingizio kuwa matumizi ya vyandarua vyenye dawa ndio chanzo.
Amesema upendo hekima na huruma ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kunusuru wananchi wake kwa kusambaza vyandarua katika wilaya hiyo ni juhudi ambazo haziwezi kufifishwa na imani potofu.
Akizungumza jana mkoani Tabora wilayani Kaliua Dk. Rashidi amewataka wananchi hao hususani vijana kutafuta mbadala wa tatizo la nguvu za kiume, ikiwemo kuzingatia vyakula vya lishe na kuacha kisingizio kuwa matumizi ya vyandarua vyenye dawa ndio chanzo.
“Kama mashine haifanyi kazi haifanyi tu sio kwa sababu ya kutumia vyandarua vyenye dawa, tutafute chanzo cha wanaume wengi kuwa na changamoto ya nguvu za kiume, sisi wengine tumetumia hivyo vyandarua miaka na miaka na hadi watoto zetu wanatumia na hatuna hiyo shida,”alisema.
Alieleza, ujio wa vyandarua hivyo ni muhimu hivyo wananchi wanatakiwa kuunga mkono jitihada hizo lengo ni kujilinda dhidi ya malaria ambayo ni tishio.
Alithibitisha ya kwamba Tabora ikiwa ni ya kwanza kitaifa kwa maambukizi ya malaria, Kalihua ni miongoni mwa wilaya zinazoongoza mkoani humo kutokana na maambukizi ya ugonjwa huo.
Alisema, uchunguzi wa afya unaonyesha kati ya watoto 10 saba wana maambukizi ya malaria hatua ambayo serikali imeona ipo haja kuongeza nguvu katika mapambano hayo ili kuwa na watu wenye afya njema.
“ Wapo watu hawana uelewa wanapotosha jamii na kusema vyandarua hivyo vinapunguza nguvu za kiume, hakuna ukweli wa dawa zinazotumika kuzuia mbu katik vyandarua kupunguza nguvu naomba mjue kuwa malaria ni hatari hivyo, nawasihi wananchi tumieni vyandarua hivi ipasavyo,”alisisitiza.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa MSD Kanda ya Tabora Adonizedeck Tefurukwa, alisema, MSD itahakikisha vyandarua 245, 777 vinasambazwa katika vituo 246 sawa na kaya 59,154 za wilaya ya Kaliua kama ilivyokusudiwa.
“Tutasambaza vyandarua kutoka katika ghala letu la MSD Kaliua kwa kutumia magari yetu zaidi ya 13 makubwa na madogo, lengo ni kuhakikisha mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria yanafikiwa,”alisema.
Aliongeza kuwa, MSD ikiwa ndio msambazaji mkuu wa bidhaa za afya kwa vituo 7, 000 vya umma na binafsi vilivyoidhinishwa na serikali itahakikisha inasambaza vyandarua hivyo hadi vituoni bila kujali kupanda kwa gharama za usafirishaji ikiwemo bei ya mafuta na kupanda kwa dola.
Naye Mwakikishi wa Wizara ya afya Wilfred Mwaifongo alisema, wananchi wa wilaya hiyo wapokee vyandarua na kutumia kwa lengo lililokusudiwa ikiwemo kujikinga dhidi ya malaria.
Alisema, hatua hiyo itaimarisha afya zao na kuchochea ukuaji wa uchumi katika Wilaya ya Kalihua.
Pia Diwani wa kata ya Uyumbu Ramadhani Mrisho, alieleza kuwa watahakikisha wanatekeleza maelekezo ya Rais hususani katika maboresho sekta ya afya.
Alisisitiza kuwa, viongozi wa kijiji na halmashauri hiyo hawatakuwa tayari kuona ugawaji wa vyandarua hivyo, unakwama kwa kuwa changamoto ya ugonjwa wa malaria wilayani humo inahitaji ufumbuzi wa pamoja.