Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Kamishina Msaidizi Mwandamizi David Misime amewataka Polisi Kata kushirikiana na viongozi mbalimbali walioko kwenye maeneo yao katika kuhamasisha wananchi wanao miliki silaha kinyume cha Sheria kusalimisha silaha hizo kwa hiyari.
Hayo yamesemwa Leo Oktoba 12 Mkoa wa Pwani akiwa kwenye ziara ya kikazi iliyolenga kutoa elimu kwa wananchi kuhusu usalimishaji wa silaha kwa hiyari zoezi linalofanyika nchi nzima.
Zoezi la usalimishaji wa silaha litafika ukomo Oktoba 31 mwaka huu ambapo amelekeza Polisi Kata nchini kote kutumia muda mchache uliosalia kutoa elimu na kuwahamasisha wananchi wenye kumiliki silaha kinyume na sheria za nchi haswa wananchi wanao ishi maeneo yaliyo karibu na mbuga za wanyama.
Misime ameeleza kama Kuna mtu ambaye anatambua ndani kwake kuna silaha ambayo ilikuwa ikimilikiwa na mtu ambaye alishafariki inapaswa kusalimishwa kabla ya tarehe 31 Oktoba na hawatachukuliwa hatua zozote za kisheria na kwa wale watakao kaidi baada ya hapo msako mkali utaanza na wale watakao kamatwa watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kufikishwa Mahakamani.
Aidha, amelipongeza Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani kwa kuwa miongoni mwa Mikoa inayofanya vizuri kwenye zoezi hili la usalimishaji wa silaha kwa hiyari akitolea mfano Wilaya ya Kipolisi Chalinze ambapo idadi ya silaha 11 zimekwishasalimishwa tangu zoezi hilo lilipoanza.
Kadhalika, ametoa pongezi na kuwaomba viongozi wa Dini na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa na Vitongoji kuendelea kutoa ushirikiano katika zoezi hili la usalimishaji wa silaha na Jeshi la Polisi litaendelea kushirikiana nao ili kuhakikisha linapata mwitikio mkubwa kwa Jamii.