Mhandisi wa vifaa tiba wa Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Kati Dodoma , Jumanne Mapesa (kulia) akimkabidhi boksi la dawa Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida, Paul Ndeki mjini Singida Oktoba 11, 2023. Wengine ni wafanyakazi wa hospitali hiyo.
…………………………………………………
Na Dotto Mwaibale, Singida
BOHARI ya Dawa (MSD) imetoa
vifaa tiba na dawa zenye thamani ya zaidi ya Sh. Milioni 532.4 katika Hospitali ya
Rufaa ya Mkoa wa Singida, Hospitali ya Wilaya ya Singida, Hospitali ya Wilaya ya Iramba, Hosptali ya Wilaya ya Ikungi na Kituo cha Afya cha
Halmashauri ya Wilaya ya Itigi kwa ajili ya kuboresha huduma za matibabu mkoani
hapa.
Akizungumza Oktoba 11, 2023 wakati wa kukabidhi
vifaa hivyo kwenye hospitali hizo, Mhandisi wa vifaa tiba wa MSD Kanda ya Kati Dodoma , Jumanne Mapesa alivitaja
vifaa tiba na dawa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida
kuwa ni vitanda 9 (ICU Beds) vya kisasa pamoja na dawa..
Alisema kwa Hospitali ya Wilaya ya Singida vifaa vilivyotolewa ni vitanda viwili wakati kwa Kituo cha Kituo cha
Afya cha Halmashauri ya Wilaya ya Itigi ni pasi ya kunyoshea nguo, vitanda vya wagonjwa, vitanda vya kujifungulia, mashuka, magodoro na viti mwendo..
Mapesa alisema utoaji wa vifaa hivyo ni
muendelezo wa uboreshaji wa huduma za sekta ya afya mkoani Singida kwani Machi 15,
2023 MSD ilitoa mashine za kufulia, vifaa vya kinywa na meno, usingizi na vitanda Hosptali ya Wilaya ya Singida Ilongero.
Baada ya kukabidhi vifaa hivyo, Wataalam kutoka MSD walitoa maelekezo kwa wataalam ambao hospitali zao zimenufaika na vifaa hivyo wavitunze ili vidumu muda mrefu kwani Serikali chini ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan imekuwa
ikitumia fedha nyingi kuvinunua.
“Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi
kununua vifaa hivi hivyo ni wajibu wa watumishi wa sekta ya afya kuhakikisha
vinatunzwa vizuri,” alisema .Mfamasia wa Kanda na Afisa Huduma kwa Wateja MSD Kanda ya Kati Dodoma, Michael Mwakuna.
Viongozi wa Hospitali hizo wameishukuru serikali
kupitia MSD kwa kuendelea kuwapatia dawa na vifaa tiba kwa wakati jambo ambalo
limeongeza tija na ufanisi wa kazi katika utoaji huduma za afya
Nao Kaimu Mganga Mfawidhi wa
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida, Paul Ndeki, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya
Singida, Yusuph Kitinya, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Itigi, Emmanuel Mallange, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Ikuni, Kahabi Kimotoli na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Hussein Sapoko waliahidi kuvitunza na kumshukuru Rais Samia kwa kuendelea kuboresha huduma za afya nchini.
“Vifaa tulivyopatiwa vitatusaidia kutoa huduma zetu tunawashukuru Serikali kwa kufanikisha upatikanaji wa vifaa tiba kupitia MSD hivyo kuhimarisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.,.” alisema Kitinya.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Ikungi, Kahabi Kimotoli alisema wamepokea vitanda 16 na kufikisha idadi ya vitanda 80 na kueleza kuwa mbali ya vifaa hivyo pia walipokea baadhi ya vifaa vingine vingi kama magodoro, mashuka, taa za kufanyia uchunguzi, taa ya chumba cha upasuaji na sasa wapo kwenye mchakato wa kupelekewa mashine itakayosaidia kufanya operesheni ya mama na mtoto katika jengo ambalo lipo mbioni kukamilika.
.“Kwa ujumla ni idadi kubwa ya vifaa tulivyoletewa na Serikali chini ya mama yetu kipenzi Rais Samia kupitia MSD.” alisema Dk.Kimotoli..
Kwa upande wake Mganga wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Hussein Sepoko alisema Rais Samia amewapelekea vifaa tiba vingi vya kisasa na akaishukuru MSD kwa ushirikiano inayowapa wa kuwapelekea vifaa tiba na dawa kwa wakati.
Nao Diwani wa Kata ya Ilongero Issa Mwiru na Diwani wa Kata
ya Itigi Mjini, Ally Minja walipongeza Serikali na MSD kwa kusambaza vifaa tiba na dawa.
“Kwa nafasi ya kipekee tunaishukuru MSD wamekuwa na ushirikiano mkubwa tunapohitaji
vifaa tiba na dawa wanatuletea kwa wakati hakika wameendelea kufanya
maboresho makubwa katika sekta ya afya ,” alisema Mwiru.
Aidha, Mwiru aliishukuru Serikali kwa kuwaletea
watumishi katika hospitali mpya ya Wilaya ya Singida na kusifia utendaji kazi
wao kwa masaa yote wanapokuwa kazini.
Leo Oktoba 12, 2023 MSD wamemaliza kufanya kazi ya kusambaza vifaa tiba na dawa katika Hospitali ya Wilaya ya Iramba Kiomboi na Ikungi hata hivyo wataendelea kufanya hivyo kulingana na mahitaji ya vifaa hivyo. .
Mashine ya kufulia nguo iliyotolewa na MSD ukiwa Hospitali ya Wilaya ya Singida