NA VICTOR MAKINDA, MOROGORO
Jeshi la Polisi Tanzania, limewataka watu wote wanaomiliki silaha pasipo kuwa na vibari, kutumia msamaha wa usalimishaji silaha kwa hiyari, kusamilisha silaha hizo kwenye vituo vya polisi kote nchini.
Wito huo umetolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, David Misime, alipozungumza na waandishi wa habari mjini Morogoro , Mkoani Morogoro mapema leo.
Misime alisema kuwa kwa mujibu wa sheria ya usimamizi na udhibiti wa silaha na risasi ya mwaka 2015 sura ya 223 kifungu 64 kinampa mamlaka Waziri wa Mambo ya ndani kutangaza msamaha wa urejeshwaji wa silaha kwa hiyari.
“Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ilitoa tangazo kwenye gazeti la serikali namba 619 la Tarehe 25.8.2023 kutoa msamaha wa usalimishaji wa silaha kwa hiyari katika kipindi cha kuanzia Tarehe 1.9.2023 hadi tarehe 31.10.2023, hivyo ninawataka watu wote wanaomiliki silaha kama vile gobole, shortgun na bunduki nyingine za aina mbali mbali, pasipo kuwa na vibari maalumu vya umiliki wa silaha kurejesha silaha hizo kwa hiyari ndani ya kipindi kabla ya tarehe 31 mwezi wa 10 mwaka huu” Alisema Misime.
Aliongeza kusema kuwa baada ya muda huo wa msahama wa urejeshaji wa silaha kwa hiyari kwisha, Jeshi la Polisi nchini litafanya msako mkali kubaini watu wote wanaomiliki silaha kinyume na sheria na kuwachukulia hatua kali za kisheria.
“ Ukirejesha silaha ndani ya kipindi hiki cha msamaha, hutochukuliwa hatua yoyote, ikiwa utapuuza agizo hili baada ya muda huo kwisha utakamatwa na kushitakiwa ambapo adhabu kwa mtu anayekutwa na hatia ya kumili bunduki na risasi kinyume na sheria ni kifungo cha miaka 15 jela au faini ya Shilingi Milioni 10 au adhabu zote kwa pamoja, hivyo ni vema watu wanaomiliki silaha hizo kinyume na sheria kutumia fursa hii kuziejesha kwa hiyari. Alisema Misime.