Wito umetolewa kwa Viongozi wa Serikali, wataalam na Maofisa Elimu ya Watu Wazima kutafuta namna ya kutambua mahitaji ya wananchi mahali walipo ili elimu nje ya mfumo rasmi inayotolewa iweze kuwanufaisha watu wengi zaidi.
Wito huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Elimu Msingi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEM, Josephat Damas Luoga alipokuwa anazindua Kituo cha Jamii cha Kujifunzia (Community Learning Center) kilichopo Ruvu JKT kata ya Mtambani, Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha.
Josephat amesema TAMISEM wana dira ya elimu ambayo ina lengo la kuwa na Mtanzania aliyeelimika, mwenye maarifa, stadi na mtazamo chanya kwa ajili ya kujiletea maendeleo yake binafsi, jamii pamoja na Taifa.
“Jitihada za Serikali katika kuendeleza dira hii imeweka mfumo wa elimu rasmi na elimu nje ya mfumo rasmi na kupitia elimu nje ya mfumo rasmi ndiyo tumewekeza kwenye vituo hivi ili watu wazima ambao hawakupata elimu waweze kuipata kulingana na mazingira waliyopo,” alieleza.
Kadhalika, aliitaka jamii iepuke watu wanaotoa tafsiri potofu kuhusu elimu ya watu wazima na waelewe kwamba elimu hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya sasa na baadaye.
Josephat alishukuru Shirika la DVV International kwa kuwajengea kituo cha kisasa ambacho kitawasaidia watu wa Kibaha Vijijini kupata Elimu nje ya mfumo rasmi.
Akizungumza katika uzinduzi huo Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson Simon amelishukuru Shirika la DVV International kwa kuwajengea kituo cha kisasa cha kutolea elimu ya watu wazima na kuwataka wananchi kukitumia kituo hicho ili kupata elimu zaid.
“Mmi ni shabaki mkubwa wa kuboresha ubinadamu, moja ya njia ya kuboresha ubinadamu ni kujifunza kuandika na kusoma. Kujifunza tunaboresha mazuri ya ubinadamu wetu na tunadhibiti mabaya ya ubinadamu wetu.” Alisema Nickson.
Mkurugenzi wa DVV International Tanzania, Frauke Heinze ameishukuru Serikali ya Jamuhuri wa Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano wanaowapa katika kuendeleza elimu ya watu wazima na kusema kwa sasa wanashirikiana katika kuhuisha na kufufua mwongozo wa ufundishaji wa watu wazima (MUKEJA).
Pamoja na kuhuisha MUKEJA, Frauke amesema kituo kilichozinduliwa kitatoa elimu zaidi ya kusoma na kuandika kwani jamii za kimataifa na Tanzani zinasisitiza watu kuwa na stadi zaidi ya kusoma, kuandika na kuhesabu.
Asha Omary, mkazi wa Mlandizi, Pwani ameishukuru Serikali kwa kuazisha mfumo wa elimu ya watu wazima kwani alikuwa hajui kusoma na kuandika jambo lililokuwa linampa changamoto kwenye biashara zake.
Asha amesema amesoma elimu hiyo kwa miezi sita na sasa amehitimu na kupata cheti ambapo ametoa wito kwa wanawake kujitokeza wanaposikia fursa kama hizo na kuachana na dhana ya uoga kwani elimu haina mwisho.