Kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Mbalali mkoani Mbeya Zainabu Lyelly,akijaribu kufungua moja katika moja ya vituo vya kuchotea maji katika kijiji cha Itipingi vilivyojengwa kupitia mradi wa maji wa Luduga-Mawindi uliotekelezwa na Ruwasa kwa gharama ya zaidi ya Sh.bilioni 5.2,wengine wanaoshuhudia na viongozi wa chombo cha watumia maji(CBWSOs).
Kaimu meneja wa wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) wilaya ya Mbalali mkoani Mbeya Zainab Lyelly kulia,akimtwisha ndoo ya maji mkazi wa kijiji cha Itipingi ambaye hakufahamika jina lake mara moja,baada ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa maji Luduga-Mawindi.
Baadhi ya viongozi wa chombo cha watumia maji wa kijiji cha Itipingi Halmashauri ya wilaya Mbalali mkoani Mbeya wakiwa katika Picha ya pamoja na kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Mbalali Zainab Lyelly wa tatu kulia baada ya kutembelea mradi wa maji wa Luduga-Mawindi ambao ukikamilika utahudumia zaidi ya wakazi 12,000.
Kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Mbalali mkoa wa Mbeya Zainab Lyelly aliyeinama,akiwaonyesha baadhi ya viongozi wa jumuiya ya watumia maji wa kijiji cha Itipingi wilayani humo baadhi ya miundombinu ya maji iliyojengwa katika mradi wa maji wa Luduga-Mawindi.
Na Muhidin Amri,
Mbalali
WAKAZI wa kijiji cha Itipingi kata ya Mawindi wilaya ya Mbalali mkoani Mbeya,wamepata matumaini ya kupata huduma ya maji safi na salama kufuatia wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)kuwa katika hatua ya mwisho kukamilisha mradi wa maji wa Luduga-Mawindi.
Kaimu Meneja wa Ruwasa wilaya ya Mbalali Zainabu Lyelly alisema,mradi huo unatarajiwa kuhudumia wakazi 12,120 wa kijiji hicho na vijiji vya Manienga,Mkandami,Matemela na Ipwani ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 88.
Alisema,mradi ulianza kutekelezwa mwezi April 2022 na ulitakiwa kukamilika mwezi Oktoba 2022,lakini kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo kuchelewa kwa malipo utakamilika mwishoni mwa mwezi huu.
Alitaja gharama ya mradi ni Sh.bilioni 5,232,737,680.93 zilizotolewa na Serikali kupitia mfuko mkuu wa serikali pamoja na mfuko wa Taifa wa maji na tayari mkandarasi amelipwa kiasi cha Sh.bilioni 3,645,405,919.64.
Alisema,kazi zilizofanyika katika ni kuchimba mitaro,kulaza bomba zenye vipenyo mbalimbali urefu wa kilomita 84.6,ujenzi wa matenki matano yenye uwezo wa kuhifadhia lita 475,000 za maji ,ujenzi wa vituo 44 vya kuchotea maji na ujenzi wa ofisi ya jumuiya ya watumia maji(CBWSOs).
Mwenyekiti wa kijiji cha Itipingi Alphonce Delile alisema,tangu uhuru wananchi wa kijiji hicho hawajawahi kuona maji ya bomba yakitoka kwenye maeneo yao, badala yake walitegemea kupata maji kwenye mito na visima vya asili ambavyo maji yake hayakuwa safi na salama.
Alisema,hali hiyo imetokana na hali ya ukame kwa muda mrefu uliosababishwa na jamii ya wafugaji wanaofanya shughuli zao kwenye mabonde na vyanzo vingine vya maji.
Alisema,mradi umesaidia sana kupunguza adha ya wananchi kutembea umbali mrefu na kutumia muda mwingi kwenda kutafuta maji kwa ajili ya matumizi yao ya kila siku na kushindwa kufanya shughuli za zingine za maendeleo.
Afisa Tabibu wa kituo cha afya Mawindi Baraka Sunyayi alisema,tangu mradi ulipoanza kutoa huduma ya maji safi na salama umesaidia kupunguza magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya maji yasiyo safi na salama ikiwemo homa za matumbo,kuharaisha na kipindu pindu.
Sunyayi ambaye ni mjumbe wa chombo cha watumia maji(CBWSOs),ameishukuru serikali ya awamu ya sita kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi huo ambao ni mkombozi kwa wananchi hasa akina mama na watoto ambao ndiyo wahanga wakubwa pindi maji yanapokosekana.
Aliongeza kuwa,mradi huo ni kama ndoto kwani wananchi wa kijiji hicho hawakuwahi kufikiri kama ipo siku watapata maji ya bomba kama ilivyo katika maeneo mengine hapa nchini.
Amewapongeza wataalam wa Ruwasa ngazi ya wilaya na mkoa wa Mbeya kwa kutekeleza mradi huo muhimu ambao unakwenda kuchochea kukua kwa uchumi na kuharakisha maendeleo ya wananchi.
Kwa upande wake mhasibu wa chombo cha maji Luduga-Mawindi Grace Mkusa alisema,kwa sasa makusanyo ya fedha za maji yanafikia Sh.milioni 3.5 kwa mwezi nje ya madeni wanayodai kwenye taasisi na idara za serikali.
Alisema,katika uendeshaji wa mradi huo changamoto kubwa ni uharibifu wa miundombinu unaofanywa na wananchi wa vijiji vingine ambavyo havijafikiwa na mradi huo na hivyo kulazimika kutumia fedha nyingi kwa ajili ya kufanya matengenezo ya miundombinu