Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila ametoa maagizo hayo leo Octoba 12, 2023 kwa wakala wa mabasi yaendayo haraka (DART) alipotembelea kuona ufanisi wa mabasi hayo katika kutoa huduma kwa wakazi wa Dar es Salaam.
RC Chalamila amesema mtoa huduma amekuwa akilipwa fedha katika mradi huo hivyo sio vema kuwa na idadi kubwa ya mabasi ambayo ni mabovu huku mahitaji kwa wananchi ni makubwa. ” Baada ya wiki mbili nataka kuona mabasi hayo yote 70 yanarudi barabarani ili kupunguza adha kwa wananchi” Alisema Chalamila
Aidha Mhe Chalamila amesema hayuko tayari kuona jitihada na dhamira njema ya Rais Dkt Samia Suluhu kwa wananchi zinakwamishwa kwa sababu ya uzembe wa watu fulani kutimiza majukumu yao.
Mhe Rais Dkt Samia ameelekeza nguvu kubwa katika kuboresha miundombinu ya barabara hususani Mwendokasi katika Mkoa huu lengo likiwa ni kuwaletea wananchi maendeleo, wapate urahisi wa kwenda hapa pale wakifanya biashara zitakazowezesha kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja na hatimaye Taifa kwa ujumla.
Vilevile Mkuu wa Mkoa ameahidi kuendelea kujifunza kwa kipindi cha wiki moja namna mabasi hayo yanavyotoa huduma kwa wananchi na kero zote walizotoa zimepokelewa.
Mwisho RC Chalamila ametumia usafiri huo mapema leo akianzia Jangwani, Kimara mwisho, Mbezi hadi Mloganzila katika sehemu zote alikua akisikiliza kero na maoni ya Wananchi juu ya namna mabasi hayo yanavyotoa huduma